RSF iliwaua wanawake 300, kubaka 25 katika saa 48 za kwanza Al Fasher: waziri wa Sudan

Wanawake ''wamedhalilishwa kingono, vurugu, na mateso" na RSF, ikiwemo waandishi wa habari wa kike, waziri wa nchi masuala ya jamii amesema.

Waziri wa Sudan anasema kama RSF itabaki Al Fasher, wataangamiza watu wote Darfur, mauaji ya kikabila;kukaa kimya ni kushiriki. / AP

Wapiganaji wa RSF wamewaua wanawake 300 na kuwabaka wanawake wengine 25 katika siku zao mbili za kuingia mji wa Al Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini magharibi mwa Sudan, waziri wa Sudan amesema.

“RSF imewaua wanawake 300 siku mbili za kwanza walipoingia Al Fasher,” Waziri wa Nchi wa Masuala ya Jamii Salma Ishaq ameiambia Anadolu.

Amesema kuwa wanawake Al Fasher “wamenyanyaswa kingono, kufanyiwa vurugu, na kuteswa” kabla ya kuuawa.

“Wanawake wote waliouawa mjini walipitia unyanyasaji wa kingono na mauaji. Hakuna mwanamke ambaye yuko salama, hata watoto,” waziri huyo alisema, akieleza kuwa matukio ya ubakaji yamefika 25.

“Kuna taarifa za waandishi wa habari wa kike kubakwa, na uhalifu huu wameufanya wazi,” aliongeza.

“Unyanyasaji wa kingono ulilenga hata watoto mbele ya mama zao, ambao waliuawa. Kila mtu ameona matukio haya kwenye video,” waziri huyo alisema.

“Yeyote anayeondoka Al Fasher kuelekea Tawila (Darfur Kaskazini) yuko hatarini, kwa kuwa barabara kati ya miji hii miwili imekuwa ‘barabara ya kifo’,” Ishaq amesema, akionesha mateso kwa wanawake na matamshi ya kibaguzi.

“RSF inatumia udhalilishaji na ubakaji kama mbinu mbaya dhidi ya wanawake wanaokimbia Al Fasher.”

Waziri huyo wa Sudan anasema bado kuna familia Al Fasher ambazo zinakabiliwa na mateso, kudhalilishwa na dhulma za kingono.

“Kilichofanyika Al Fasher ni mpangilio wa maksudi wa mauaji ya kikabila, uhalifu mkubwa ambao kila mtu anahusika kwa kunyamaza kimya.”

Uhalifu wa RSF

Ishaq anasema uhalifu wa RSF Al Fasher ni sawa na mauaji ya kikatili yaliyofanyika Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi 2023.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Januari 2024 watu kati ya 10,000 na 15,000 waliuawa Geneina, ikiwemo gavana wa jimbo, katika mauaji ya kikabila yaliyofanywa na RSF na wapiganaji washirika.

“Bila shaka, yaliyotokea Geneina hayako kwenye video vizuri kama ilivyokuwa Al Fasher. Video za RSF wenyewe Geneina hazikuwa na muonekano mzuri kama ilivyo Al Fasher,” Ishaq amesema.

Waziri huyo amesisitiza kuwa video za uhalifu wa RSF zimekuwa “sehemu ya waasi hao kutumia kama silaha kupata ushindi dhidi ya upande mwingine.”

“Furaha ya kuua yenyewe inawapa hisia za ushindi. Kisaikolojia, ni ugonjwa wa aina fulani wa kupata ushindi. Ni kama kumkabili mpinzani wako kwa mafanikio, na hali hii imekuwa sehemu muhimu ya silaha kwa RSF,” aliongeza.

“Kama RSF imebaki Al Fasher, watamuangamiza kila binadamu Darfur. Haya ni mauaji ya kikabila, na kila mtu anahusika kwa kukaa kimya,” waziri huyo alionya.

Alisisitiza kuwa kukaa kimya kwa jamii ya kimataifa kutawapa nguvu RSF kuendeleza uhalifu huko Al Fasher na nchini kote.

Mashirika ya misaada Al Fasher, Ishaq anasema misaada iliyofikishwa Tawila kupitia mashirika mengine haitoshi kukidhi mahitaji ya maelfu ya familia zilizokimbia makazi yao katika mji huo.

Alieleza kuwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanashindwa kuingia eneo hilo, kwa kuwa ni hatari kwa maisha ya raia na wafanyakazi wengine wa misaada.

“Lakini tunawasiliana na wadau wote na kujaribu kusaidia kupeleka fedha bila kutangaza ,” alisema.

Oktoba 26, RSF ilidhibiti Al Fasher na kutekeleza “mauaji ya kikatili” dhidi ya raia, kulingana na mashirika ya eneo hilo na kimataifa, huku kukiwa na onyo kuwa mauaji hayo yanawexa kuleta mgawanyiko mkubwa nchini Sudan.

Siku ya Jumatano, kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo (Hemetti) alikiri kuwa kulikuwa na “ukiukwaji” kutoka kwa wapiganaji wake Al Fasher, akidai kuwa kamati za uchunguzi zimeundwa.

Kwa wao kudhibiti Al Fasher, RSF imepata kudhibiti majimbo yote matano ya Darfur huko magharibi, kati ya majimbo 18 ya Sudan, huku jeshi la nchi likidhibiti maeneo mengi ya majimbo 13 yaliyobaki kusini, kaskazini, mashariki, na katikati, ikiwemo mji mkuu wa Khartoum.

Eneo la Darfur ni humusi ya nchi nzima ya Sudan, lakini wengi ya raia milioni 50 wa nchi hiyo wanaishi katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi.

SOURCE: AA