Serikali ya Marekani imetoa zaidi ya dola milioni 1 za Kimarekani kupitia fungu jipya la kuisaidia Serikali ya Tanzania kuimarisha maandalizi na utayari wake wa kukabiliana na Ebola.
Msaada huo, unatolewa kufuatia milipuko ya ugonjwa huo nchini DRC na Uganda.
Kulingana na taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, msaada huo unalenga kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, mifumo ya maabara, kinga na udhibiti wa maambukizi.
Pia, utalenga usimamizi wa wagonjwa, mawasiliano kuhusu hatari ya mlipuko na ushirikishwaji wa jamii, maandalizi katika maeneo ya kuingilia nchini, uratibu wa dharura na kuimarisha nguvu kazi katika mikoa iliyo katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi ya kutoka nchi jirani.
“Uwekezaji huu unaendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Marekani na Tanzania katika kuimarisha mifumo ya usalama wa afya yenye uwezo wa kuzuia, kugundua na kukabiliana kwa haraka na vitisho vinavyoibuka vya maradhi ya kuambukiza,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

















