Kipenga cha mwisho kilipopulizwa na kuitangaza Hispania kuwa mabingwa wa dunia baada ya kuilaza Argentina bao 1-0 kwenye fainali za Kombe la Dunia, kule nchini Marekani, macho ya wengi yalielekezwa kwa wachezaji.
Lakini kwa Nico Williams, kulikuwa na ushindi mmoja mkubwa zaidi ya kombe lenyewe.
Badala ya kuwakimbilia wachezaji wenzake na kuwakumbatia au kuinua kombe mbele ya mashabiki, winga huyo mwenye kasi ya radi alimtafuta mtu mmoja pekee... mama yake, María Williams.
Alipomfikia, bila kusita alimvisha medali yake ya dhahabu.
Uwanja mzima ukasimama kushuhudia tukio lililogusa mioyo ya wengi.
María, aliyekuwa amevaa jezi ya Hispania akiwa jukwaani, alishindwa kujizuia kutoa machozi.
Hayakuwa machozi ya furaha pekee, bali ya safari ndefu ya mateso, matumaini na ushindi.
Nico alimkumbatia mama yake kwa nguvu na kwa sauti ya hisia akasema kwa Kihispania: “Tumefaulu.”
Alijua ushindi huo haukuwa ni wake peke yake, bali ulikuwa wa familia nzima.
Na kweli, uchungu wa mwana aujuae ni mama.
Miaka mingi iliyopita, María Williams na mume wake Félix waliondoka Ghana wakikimbia umaskini na kutafuta maisha bora Ulaya.
Safari yao haikuwa ya ndege wala basi. Walivuka Jangwa la Sahara kwa miguu, wakihatarisha kila hatua ya maisha yao.
Walipofika Melilla, eneo la Hispania lililopo Kaskazini mwa Afrika, walikamatwa na kuwekwa kizuizini. Wakati huo María alikuwa na ujauzito wa mtoto wao wa kwanza, Iñaki Williams.
Licha ya kushinikizwa warudi walikotoka, walikataa. Hatimaye waliruhusiwa kuingia Hispania na kufika Pamplona wakiwa hawana chochote zaidi ya matumaini.
Muda mfupi baadaye Iñaki akazaliwa. Kisha mwaka 2002 wakampata Nico.
Maisha hayakuwa rahisi. Kulikuwa na mapambano ya kila siku, lakini ndoto ya mafanikio haikufifia.
Wazazi waliendelea kujitolea, huku watoto wao wakikimbizana na mpira kwenye viwanja vidogo wakiamini ipo siku wataibadilisha historia ya familia yao.
Bahati ikagonga mlango
Athletic Bilbao ikamchukua Iñaki, na baadaye Nico naye akafuata nyayo za kaka yake. Vipaji vikachanua, majina yao yakaanza kutikisa soka ya Hispania.
Ingawa ndugu hao walifuata njia tofauti kwenye timu za taifa, walifanya hivyo kwa heshima ya wazazi wao.
Iñaki aliichagua Ghana mwaka 2022 ili kuenzi chimbuko la familia yao, huku Nico akiitumikia Hispania, nchi aliyozaliwa.
Aliitwa kwa mara ya kwanza kikosini mwaka 2022, akawa sehemu ya kikosi kilichotwaa Euro 2024, na sasa ameandika historia nyingine kwa kutwaa Kombe la Dunia.
Kutoka kwenye jangwa lenye kiu na mateso, kupitia vizuizi vya uhamiaji na maisha ya shida, hadi kilele cha soka duniani... hiyo ndiyo safari ya familia ya Williams.
Ndiyo maana, baada ya ushindi huo wa kihistoria wa Julai 19 dhidi ya Argentina, Nico hakutafuta kamera, hakutafuta makofi wala sifa.
Alimtafuta mama yake.
Kwa sababu alijua, medali hiyo ya dhahabu haikuanza kutengenezwa katika uwanja wa MetLife Stadium.
Ilianza kutengenezwa kwenye mchanga wa Jangwa la Sahara, ikapitia machozi ya María Williams, na ikakamilika shingoni mwa mwana aliyekumbuka alikotoka.
Kweli, liandikwalo na Mola halifutiki.


















