| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Uganda inasema uchumi wake uko imara licha ya misukosuko ya dunia
Mwaka 2025 Uganda ilipata dola za Marekani bilioni 14.4 katika mauzo ya nje ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kuingiza kiasi hicho kupitia mauzo ya nje.
Uganda inasema uchumi wake uko imara licha ya misukosuko ya dunia
Serikali ya uganda inasema uchumi wa nchi uko thabiti / Reuters
tokea masaa 2

Katibu wa Hazina wa Uganda, Ramathan Ggoobi amefichua kuwa licha ya uchumi wa Uganda kukabiliwa na mfumuko wa bei baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita, mwaka huu umeendelea kuwa tulivu.

Anasema licha ya matukio ya kimataifa, kama vile mgogoro wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, uchumi wa nchi hiyo bado ni imara.

"Uchumi wa Uganda unafanya vizuri sana licha ya masuala yote yanayotokea, majanga ndani ya nchi, nje ya nchi. Nadhani ni moja ya nyakati chache katika historia ya Uganda ambapo tumekuwa na uchumi madhubuti wakati wa msimu wa kisiasa. Hata kipindi cha mvutano wa kisiasa haukuathiri utendaji wetu kama inavyoonyeshwa na viashiria kadhaa," alifafanua Ggoobi.

Aliyasema hayo alipokuwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambapo aliitwa kujibu hoja zilizotolewa kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Wizara ya Fedha ya Disemba 2025.

"Shilingi pia ni madhubuti na yenye nguvu dhidi ya sarafu za kigeni. Imekuwa ikiimarika dhidi ya dola na sarafu nyingine kuu hasa kwa sababu ya utendaji mzuri wa mauzo ya nje,” alifafanua.

“Mwishoni mwa mwaka uliopita, Disemba, utendaji wetu wa mauzo ya nje nchini Uganda ulifikia kiwango ambacho hakijawahi kuonekana katika historia yake. Tulipata mauzo makubwa ya bidhaa na huduma za Dola za Marekani Bilioni 14.4 (UGX53.643 Trilioni).

Mapato ya kigeni yanaimarika

Aliendelea kusema kuwa mwaka 2025, Uganda ilipata dola za Marekani Bilioni 14.4 (UGX53.643 Trilioni) katika mauzo ya nje ikiwa ni mara ya kwanza kwa Uganda kupata kiasi hicho kupitia mauzo ya nje.

Anasema ukuaji wa Pato la Taifa unachangiwa na utendaji thabiti katika sekta zote za uchumi ikiwemo kilimo, viwanda na sekta ya huduma.

Malengo ya nchi ni kukua kati ya asilimia 6.5 na 7 mwaka huu wa fedha.

Katibu wa Hazina pia aliripoti kwamba akaunti ya fedha ya Uganda inafanya vizuri na kwamba mapato yalikuwa ya Dola za Kimarekani Bilioni 5.6 ambapo Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Kigeni ulikuwa wa Dola za Kimarekani Bilioni 3.56 wakati kwengineko kwa wawekezaji ilikuwa karibu Dola za Kimarekani Bilioni 1.7.

"Matokeo yake, shilingi imebaki kuwa imara. Dola inapatikana kwa kila mtu. Matokeo yake ni kuwa salio letu la malipo lilisajili ziada ya Dola za Marekani Bilioni 2.37 mwishoni mwa Oktoba 2025. Hii inaashiria kwamba Uganda ilipata pesa zaidi ya ile iliyotoka Uganda kwa Bilioni 2 za Marekani," aliongeza.

Ggoobi hata hivyo, alikiri kwamba bado kuna udhaifu katika ukusanyaji wa mapato ambayo yanazuia maendeleo ya kiuchumi ya Uganda.

CHANZO:TRT Swahili