Uimarishaji wa Uturuki ni heshima na kumuenzi Ataturk: Erdogan

Rais wa Uturuki amemuenzi mwanzilishi huyo wa jamhuri akitangaza ufunguzi wa eneo alilozaliwa Ataturk.

By
Ataturk aliongoza mapambano ya Uturuki ya kudai uhuru pamoja na kuanzisha jamhuri mwaka 1923.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan siku ya Jumatatu, aliongoza adhimisho la miaka 87 ya kifo cha Mustafa Kemal Ataturk, baba wa taifa na mwanzilishi wa jamhuri ya Uturuki.

Akizungumza wakati wa adhimisho hilo, Erdogan alimuenzi Ataturk, akiwashukuru wanachama wa kwanza wa Bunge la Taifa, ambao waliongoza mapambano ya uhuru na uanzishwaji wa dola mpya ya Uturuki.

Pia, alitoa heshima kwenye kumbukumbu ya mashahidi wa taifa—wakiwemo wale wa ukombozi wa Istanbul na mapambano ya Canakkale na mashujaa wa Julai 15 ambao walizima jaribio la mapinduzi.

Akinukuu kauli maarufu ya Ataturk, “Siku  moja, mwili wangu utageuka kuwa mavumbi, lakini Jamhuri ya Uturuki itaendelea kuwepo,” Erdogan alisema kauli hiyo inasadifu maono ya mwanzilishi kwa ajili ya taifa imara.

 “Kumuenzi Ataturk inamaanisha kuimarisha jamhuri yetu na kuifanya iwe ya mafanikio katika kila nyanja,” alisema Rais Erdogan.

Ugiriki, alikozaliwa Ataturk

Katika hatua nyingine, Erdogan alitangaza kukamilika kwa ukarabati wa miezi 11 wa eneo alilozaliwa Ataturk huko Thessaloniki nchini Ugiriki, mchakato uliotaribiwa na Wizara ya Utalii na Utamaduni na Shirika la Maendeleo la Uturuki (TIKA).

“Eneo hili la kihistoria limekarabatiwa na sasa liko wazi kwa wageni na watalii,” alisema Erdogan, akielezea mradi huo kuwa ni sehemi ya jitihada za kuhifadhi urithi wa Ataturk.

Ataturk, ambaye aliongoza mapambano ya Uturuki ya kudai uhuru pamoja na kuanzisha jamhuri mwaka 1923, alifariki dunia Novemba 10, 1938, akiwa na umri wa miaka 57, ndani ya kasri ya Dolmabahce jijini Istanbul.

Kila mwaka, ifikapo saa 9 na dakika 5 asubuhi, taifa humkumbuka kiongozi huyo, likienzi mchango wake katika nchi hiyo.