Julai 9, treni mbili za mizigo zilizokuwa zimebeba kontena 98 ziliondoka Chengdu na Chongqing nchini China.
Zilipitia Kazakhstan, bahari ya Kaspi, Azerbaijan, Georgia, hadi Uturuki kwa kupitia njia ya reli ya Baku-Tbilisi-Kars, na hatimaye kuwasili katika Kituo cha Halkali cha Istanbul.
Kutoka hapo, msafara ulielekea Poland na Hungary — ikiwa ni hatua kubwa ya mafanikio ya ‘Ushoroba wa Kati’ — njia inayounganisha China hadi Ulaya kwa kupitia Katikati mwa Asia na Uturuki.
Treni za kwanza kwa njia hii ni ishara ya mradi huu muhimu, unaolenga kuunganisha mashariki na magharibi.
Huku mfumo wa biashara duniani ukibadilika, Uturuki inaibuka kama sehemu muhimu ya biashara kati ya mashariki na magharibi kupitia upanuzi wa ushoroba huo muhimu.
Wakati mmoja njia hiyo ikionekana kama isiyo na umuhimu, Ushoroba wa Kati sasa unakuwa njia mbadala inayopendwa katika reli inayodhibitiwa na Urusi na njia ya taratibu, ya gharama kubwa ya baharini kuelekea kusini.
Maafisa wa Uturuki na wataalamu katika kanda wanaeleza ushoroba huo kuwa fursa ya mabadiliko siyo tu kwa Uturuki lakini pia kwa Ulaya, China, na maeneo ya watu wanaozungumza Kituruki kote duniani.
“Uturuki inakuwa uti wa mgongo wa biashara, ambayo inaunganisha nchi 21 moja kwa moja,” Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu Abdulkadir Uraloglu alisema hivi majuzi katika kongamano jijini Istanbul.
“Njia hii ni ya mara mbili zaidi kwa haraka kwa usafiri wa baharini na gharama ya chini mara nne zaidi ukilinganisha na usafiri wa mizigo kwa ndege. Huku uwekezaji ukiendelea, tunatarajia kupunguza muda wa kusafiri kutoka Mashariki ya mbali mpaka Ulaya kwa hadi siku 13.”
Ushoroba wa Kati ni wa kilomita karibu 4,300 huku kilomita 2,200 zikiwa zinapita Uturuki.
Uraloglu ameeleza kuwa Uturuki tayari inaimarisha uwezo wa njia hiyo, ikiwemo reli mpya Istanbul na ushirikiano mkubwa wa kikanda.
“Sisi siyo tu nchi ya kupita,” alisema. “Tunatengeneza mfumo wa kimazingira katika kitovu cha Ulaya na Asia.”
Mabadiliko ya kimkakati ya biashara duniani
Msomi wa uhusiano wa kimataifa, Profesa Oktay Firat Tanrisever kutoka Chuo Kikuu cha Middle East Technical University (METU) jijini Ankara, anasema kuwa Ushoroba wa Kati ni zaidi ya suluhisho la usafirishaji; ni kujipanga kwa miungano ya kisiasa.
“Kuimarisha kikamilifu Ushoroba wa Kati kutaleta fursa nyingi sana — siyo tu kwa Uturuki bali pia kwa mataifa yanayozungumza Kituruki, lakini pia kwa Ulaya na China,” ameiambia TRT World.
“Inawapa Uturuki nafasi ya kuimarisha njia hiyo na kuwa na umuhimu wa kutoa muelekeo wa usalama na kuunganisha kanda nzima.”
Barabara mpya ya Silk katika reli ya chuma
Ushoroba wa Kati — unajumuisha reli ya Baku-Tbilisi-Kars na kuweka sawa na miundombinu kama ya TANAP — yanatajwa na wafanyabiashara duniani kama "Barabara Mpya ya Silk." Ni mfumo ambao unakubalika zaidi katika usafirishaji.
“Fursa za usafirishaji zinajulikana na kama ‘Barabara mpya ya Silk’ au ‘Ushoroba wa Kati’ katika ulimwengu wa leo wa kibiashara,” anasema Cem Kumuk, mfanyabiashara.
“Fursa hizi ni mbadala wa kuunganisha China, mmoja ya maeneo makubwa ya uzalishaji, kupeleka Ulaya, moja ya soko lake kubwa.”
Mashariki inakutana na Magharibi
Treni ya kutoka Chengdu inasafiri kilomita 10,400 hadi Lodz, Poland, huku treni ya pili kutoka Chongqing inaenda safari ya kilomita 10,998 ikipitia mji wa Budapest, Hungary.
Safari hii ya muunganisho wa reli — kupitia Mashariki mwa Ulaya na Magharibi mwa Asia na Anatolia — ni ishara ya umuhimu wa njia hiyo katika usambazaji wa bidhaa duniani.
“Umuhimu wa Uturuki katika kusafirisha mizigo mashariki hai magharibi unaimarishwa kila tunapofanikisha safari,” Waziri Uraloglu amesema. “Tumedhamiria kuimarisha hili katika kitovu cha Ushoroba wa Kati.”
Huku miundombinu ikiimarika na uwekezaji wa reli mpya ukiendelea, wataalamu wanaonya kuwa mafanikio yatahitaji zaidi ya chuma na zege.
“La msingi hapa ni ushirikishwaji,” anasema Tanrisever. “Hii njia itafanikiwa tu iwapo kutakuwa na utashi wa kisiasa, miungano ya kikanda, na diplomasia thabiti inayoendana na uhandisi.”
Na wakati biashara inapoongeza matawi na kubadilika, Uturuki siyo tu ni kiunganishi muhimu kati ya Asia na Ulaya — ni njia muhimu ya usafiri, diplomasia, na muelekeo wa biashara katika karne ya 21.



















