Umati wa watu waliokuwa na shauku katika nchi hiyo yenye Wakatoliki wengi walijipanga kando ya barabara kutoka uwanja wa ndege kuelekea mji mkuu Malabo, wakimshangilia papa wa kwanza kutembelea nchi hiyo tangu Mtakatifu Yohane Paulo II mwaka 1982.
Nchi hiyo ya zamani ya koloni la Hispania katika pwani ya magharibi ya Afrika inaongozwa na rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani humo, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo.
Ugunduzi wa mafuta baharini katikati ya miaka ya 1990 uliibadilisha kwa haraka sana uchumi wa Equatorial Guinea, huku mafuta sasa yakichangia karibu nusu ya pato lake la taifa (GDP) na zaidi ya asilimia 90 ya mauzo ya nje, kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Papa Leo XIV, ambaye amewasili Equatorial Guinea, akitokea nchini Angola, alikutana Rais Teodoro Obiang Nguema katika Ikulu ya nchi hiyo, kabla ya kuwahutubia viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wawakilishi wa utumishi wa umma.. Akibainisha kuwa mkutano huo ulifanyika katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha Papa Francis, Papa Leo alinukuu maneno ya papa huyo marehemu akilaani pengo la kipato alilosema limezidishwa na uchumi wa dunia unaolenga faida kwa gharama yoyote.
“Uchumi wa namna hiyo unaua,” alisema Leo. “Kwa hakika, leo hii inaonekana wazi zaidi kuliko miaka iliyopita kwamba kuenea kwa migogoro ya silaha mara nyingi kunachochewa na ukoloni wa hifadhi za mafuta na madini, unaofanyika bila kujali sheria za kimataifa au haki ya watu kujitawala.”
Serikali ya Marekani, ambao umetangaza mipango ya kuunda muungano wa biashara ya madini na washirika wake, imekuwa ikiharakisha kupata ufikiaji wa maeneo yenye utajiri wa madini muhimu barani Afrika na kushindana na China katika eneo ambalo Beijing imekuwa na ushawishi mkubwa kwa muda mrefu.
Mwaka jana, wakati serikali hio ilipojitokeza kama mpatanishi muhimu wa makubaliano ya amani ya kumaliza mapigano katika eneo la mashariki mwa Congo lenye utajiri wa madini, lakini lililokumbwa na migogoro, pia ulisaini ushirikiano na Congo ambao ungeyaruhusu makampuni ya Marekani kufikia madini yake.
Marekani pia inawekeza fedha katika Ukanda wa Lobito, mradi mkubwa wa reli utakaorahisisha usafirishaji wa madini kutoka maeneo ya Zambia na Congo kupitia Lobito nchini Angola. Wakati huohuo, Marekani imeunga mkono mradi nchini Afrika Kusini unaolenga kuchimba madini adimu kutoka taka za viwandani.
















