Marekani ilisema inashirikisha mamlaka za Kenya na inaamini kwamba wasiwasi unaohusu kituo cha kutengwa kwa waathiriwa wa Ebola unaweza kutatuliwa baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kusimamisha kwa muda mradi huo siku ya Alhamisi.
"Tunafahamu kuhusu hatua ya mahakama iliyowasilishwa nchini Kenya dhidi ya kituo cha kutengwa kwa Ebola. Tunawasiliana na mamlaka ya Kenya na tuna matumaini tunaweza kutatua pingamizi," ilisema taarifa kutoka Ofisi ya Jeremy P. Lewin, katibu mdogo wa Marekani anayehusika na masuala ya kigeni, masuala ya kibinadamu na uhuru wa kidini.
Kauli hiyo ya Jumamosi ni jibu la kwanza la umma kutoka Washington tangu Mahakama Kuu ya Kenya kusitisha uanzishaji au utendakazi wa kituo kilichopendekezwa kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa ombi la kikatiba.
Jaji Patricia Nyaundi alitoa maagizo hayo ya muda baada ya kikundi cha haki za binadamu kupinga mradi huo, kikisema kuwa kiliibua masuala ya kikatiba na maslahi ya umma ambayo yanahitaji mapitio ya mahakama.
Mabishano yanapamba moto
Kituo hicho kilichopendekezwa kimezua mjadala mkali nchini Kenya kufuatia ripoti kwamba kinaweza kutumika kuhusiana na hatua za kujitayarisha za Marekani zinazohusisha raia wa Marekani ambao wanaweza kuambukizwa Ebola wakati wa mlipuko unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakosoaji wanahoji ni kwa nini kituo kinachohusishwa na mipango ya kukabiliana na Ebola ya Marekani kingepatikana nchini Kenya, wakati wafuasi wanahoji kuwa nchi hiyo imetumika kwa muda mrefu kama kitovu cha shughuli za afya ya umma, uratibu wa misaada ya kibinadamu, na ufuatiliaji wa magonjwa.
Mpinzani na aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua alikosoa kituo hicho kilichopendekezwa, akisema kuwa Kenya haifai kuwekwa katikati ya juhudi za mataifa ya nje ya kujiandaa na Ebola kwani nchi yenyewe haina mlipuko wowote uliothibitishwa.
Wataalamu wa matibabu pia wamepima mjadala huo. Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya umetaka kuwepo kwa uwazi kamili kuhusu makubaliano yoyote yanayohusiana na kituo hicho kilichopendekezwa, kikisema masuala ya afya na usalama ya umma yanapaswa kushughulikiwa kwa uwazi kabla ya mpango kama huo kusogezwa mbele.
Mamlaka ya Kenya yatetea hatua hiyo
Hata hivyo, Wizara ya Afya ya Kenya imetetea jukumu la nchi hiyo katika juhudi za usalama wa afya duniani, ikisema ushirikiano wowote wa kimataifa wa afya utasimamiwa na sheria za Kenya, kanuni za afya ya umma, na viwango vikali vya usalama wa viumbe hai.
Wizara pia ilisisitiza kuwa Kenya imeimarisha hatua za ufuatiliaji katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa uchunguzi katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege, maandalizi ya maabara na mifumo ya kukabiliana na dharura.
Maafisa wa afya nchini Kenya wamesema zaidi ya wasafiri 55,000 wamekaguliwa katika mipakan ya kuingia huku washukiwa waliopimwa nchini Kenya wakikutwa bila maambukizi.


















