| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Marekani yawawekea vikwazo makamanda wanaohusishwa na vita mashariki mwa DRC
Wizara ya Fedha ya Marekani ilisema katika taarifa kwamba imeweka vikwazo dhidi ya kamanda wa M23 na mkuu wa ujasusi, John Imani Nzenze, pamoja na Gustave Kubwayo, kamanda wa FDLR na kiongozi wa kitengo cha ujasusi na operesheni maalumu.
Marekani yawawekea vikwazo makamanda wanaohusishwa na vita mashariki mwa DRC
Waasi wa M23, wanaendelea kupigana dhidi ya FDLR, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano. / / Reuters

Marekani siku ya Jumanne imewaekea vikwazo makamanda wa makundi ya silaha ambayo imeyashutumu kwa kuchochea mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako mapigano yanaendelea licha ya juhudi za upatanishi zinazofanywa na Marekani.

Waasi wa M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, wanapigana dhidi ya FDLR, wanamgambo wa Kihutu wanaohusishwa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Hata hivyo Rwanda inaendelea kukanusha madai ya kuunga mkono kundi la M23.

Wizara ya Fedha ya Marekani ilisema katika taarifa kwamba imeweka vikwazo dhidi ya kamanda wa M23 na mkuu wa ujasusi, John Imani Nzenze, pamoja na Gustave Kubwayo, kamanda wa FDLR na kiongozi wa kitengo cha ujasusi na operesheni maalumu.

“Rais Donald Trump ameweka wazi kuwa kuna haja ya haraka ya kumaliza mzozo huu mbaya mashariki mwa DRC, na Marekani inajitahidi kuleta amani na ustawi katika eneo hilo,” alisema Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, katika taarifa hiyo.

“Vurugu zinazoendelea kufanywa na makundi yenye silaha zinazidisha mgogoro wa kibinadamu ambao tayari ni mbaya na pia zinatishia maslahi ya Marekani katika eneo hilo. Vikwazo vya leo vinaunga mkono suluhisho la amani na kukomesha umwagaji damu.”

Hadi sasa hakuna ufafanuzi wowote kutoka Nzenze, ambaye ni msemaji wa serikali ya Rwanda na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Rwanda na Congo zilitia saini makubaliano ya kusitisha vita huko Washington, Marekani mwezi Disemba kama sehemu ya juhudi za Rais Trump za kusuluhisha mgogoro huo na kuvutia uwekezaji wa mabilioni ya Dola kutoka nchi za Magharibi.

Hata hivyo, siku chache baada ya makubaliano hayo, waasi wa M23 waliingia katika mji wa mashariki mwa Congo wa Uvira, karibu na mpaka wa Burundi, katika kile kilichoonekana kuwa ongezeko kubwa zaidi la mapigano katika miezi kadhaa. Baadaye waliondoka eneo hilo kutokana na shinikizo kutoka Marekani.

CHANZO:Reuters