Uganda kuamua: Muelekeo wa Kampeni ya Uchaguzi wa 2026

Uganda inapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Januari 15, 2026, kampeni za Uchaguzi wa mwaka huu zimeonesha kwa jinsi gani wanasiasa walivyokuwa kwenye mchakato huo na kwa nini wanataka kupewa ridhaa na wananchi.

By
Mikutano ni ishara ya uwezo wa kisiasa wa vyama; inadhihirisha umaarufu, kuwahamasisha wafuasi, na inafuatilia na vyombo vya habari. / TRT Afrika

Mbali na kunadi sera zao, kampeni za mwaka huu pia zimeonesha mikakati mbalimbali iliyotumika, ikiwemo mbinu za jadi na za kisasa, zote zikiwa na lengo la kuleta ushindi katika mazingira yenye ushindani mkali.

Bila shaka, athari za mbinu hizo, zitadhihirika katika matokeo ya uchaguzi, ingawa kutumika kwake, tayari kunaleta taswira ya hali ya kisiasa ilivyo katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Kwanza ni muhimu kujua kuwa, mazingira ya kisiasa ya Uganda hayatoi fursa sawa.

Mazingira ya kisiasa ya nchi hiyo, kwa muda mrefu yamegubikwa na kubinywa kwa upinzani, na kutopewa fursa sawa ya rasilimali, hasa pale wagombea wanapofanya kampeni.

Matokeo yake sasa, sio wanasiasa wote waliokuwa na uwezo wa kutumia mbinu sawa katika kampeni.

Baadhi ya mikakati ilitumika tu kwa mgombea aliye madarakani, huku wengine wakishindwa kutumia mbinu kama hizo kutokana na vikwazo vilivyowekwa, au mipaka ya kiutawala na vikosi vya ulinzi vilivyotumika kuzuia baadhi ya wagombea wa upinzani.

Makala hii haina nia ya kulinganisha fursa au usawa waliokuwa nao wagombea. Lakini, inaangazia mbinu za kampeni za kisiasa na mikakati iliyotumika wakati wa kampeni nchini Uganda.

Mazingira ya kawaida ya kampeni nchini Uganda ni mikutano ya kisiasa.

Mikutano bado inabaki kama njia pekee ya kuonesha nguvu ya kisiasa, na kuwaruhusu wagombea kupata umaarufu, kuongeza wafuasi, na kuimarisha ngome zao.

Mziki, kauli mbiu, rangi za vyama, na matamasha hutumika kubadilisha mikusanyiko hii na kuwa sehemu ya utambulisho inayovutia kisiasa.

Kwa mfano, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine) amevutia watu katika maeneo ya mijini kama vile katika manispaa ya Kira, ambapo wafuasi walijipanga pembezoni mwa barabara kumpungia mkono alipokuwa katika ziara yake.

Wakati huo huo, chama cha National Resistance Movement (NRM) cha Rais Yoweri Museveni pia kimekuwa na mikutano mikubwa inayoashiria uwezo wake wa kuratibu mikutano.

Mikutano inahitaji rasilimali nyingi, na kutafuta wafuasi wapya, na kuibua maswali kuhusu uwezo wake wa kuwashawishi wapiga kura ambao bado hawajafanya uamuzi.

Wagombea wote wawili wanaotarajiwa kuwa na ushindani mkali nchini Uganda, Rais Yoweri Museveni na Bobi Wine, wameonekana wakihutubia mikutano ya hadhara, wakati mwengine wakisimamisha msafara katikati ya barabara, na kuonekana katika maeneo mbalimbali wanapokuwa safarini ndani ya siku moja.

Hii ni mbinu inayoonesha unyenyekevu, udhibiti, na kujumuika na watu wa kawaida.

Tofauti na mikutano ya hadhara, kusimamisha msafara ghafla, ni mkakati wa kuonesha uwezo wa simulizi zaidi kuliko kunadi sera.

Tofauti na kampeni za nyumba hadi nyumba, ambazo ni kiashiria cha ukaribu zaidi zinazolenga moja kwa moja.

Maafisa wa kampeni wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC), wameelezea umuhimu wa kampeni za mtu mmoja mmoja, ikiwemo nyumba hadi nyumba, kama sehemu ya mkakati wao mpana, unaolenga kujumuisha manung'uniko ya maisha ya watu, upatikanaji wa huduma, na gharama za maisha.

Kampeni za nyumba hadi nyumba zimetambuliwa rasmi na FDC kuwa hazina gharama kubwa na pia zinaimarisha uhusiano kati ya mgombea na wapiga kura.

Lakini, kampeni pia zimebadilishwa na mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ndio majukwaa muhimu ya kuwasilisha ujumbe wa kisiasa, hasa kwa vijana na wapiga kura wa mijini.

Kampeni za Rais Museveni na Bobi Wine zote zimetumia TikTok, Instagram, na X (iliyokuwa Twitter) kwa kusambaza video, kuonesha matukio ya kampeni, na kuonesha ushindani dhidi ya wapinzani.


Njia hii, inawawezesha wagombea kuwafikia wapiga kura moja kwa moja, na kuviacha vyombo vya habari, na kupaza sauti mbali zaidi ya mikutano ya kisiasa.

Kwa upande mwengine, matumizi ya 'podcast' na matangazo ya muda mrefu yanawawezesha wagombea kujieleza zaidi kwa kirefu.

Mfano mzuri ni podcast ya UNSTOPPABLE MUSEVENI, ambayo inamuonesha Museveni akijadili mambo kadhaa ikiwemo ukosefu wa ajira na ubunifu na vijana wa Gen Z.

Njia nyengine ya kampeni ni matumizi ya fulana, na matangazo yenye alama maalumu za vyama.

Vyote, NRM na NUP ya Bobi Wine vimekuwa vikisambaza bidhaa za kampeni ili kudhihirisha uwepo wao na utambulisho.

Matangazo ya kampeni yameenea, yakionekana katika maeneo jirani, kwenye magari, na maeneo ya umma kwa lengo la kuonesha uwepo wa mgombea.

Rais Museveni ameenda mbali zaidi na kuweka matangazo hata katika barabara kuu kama vile za uwanja wa ndege, kuonesha ni jinsi gani vyama vinatumia kila fursa kuhakikisha vinabaki katika akili za wapiga kura.

Mbali na hivyo, kuna mbinu nyengine zilizotumika, ikiwemo ile ya kuweka masanamu makubwa yenye sura za wagombea kama vile Rais Museveni, na matukio ya kidijitali kama vile "Mkutano wa muda mrefu zaidi wa mtandaoni, "Longest Online Rally."

Mikakati hii, ni ishara ya uwepo wa mgombea na ushawishi wake, na kufanya mazingira halisi na yale ya mtandaoni kama sehemu muhimu za kisiasa.

Masanamu yanavuta hisia za watu, wakati mikutano ya kupitia mitandaoni yanajumuisha watu wanaovuka mipaka wakati huo huo, kuweza kusambazwa katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.

Kinachofurahisha zaidi, ni matumizi ya mikakati tofauti na sio mkakati mmoja.

Mwishowe kabisa, ufanisi wa mikakati hii, utaonekana katika sanduku la kupiga kura. Wakati huo huo, mbali na matokeo ya uchaguzi, msimu wa kampeni nchini Uganda, unatoa funzo kubwa kuhusu mawasiliano ya kisiasa, ushirikishwaji wa wapiga kura, na ushindani.

Unaonesha mabadiliko ya kampeni ambapo mbinu za kale zinajumuishwa na ubunifu wa kidijitali.

Raia wa Uganda wanapopiga kura Januari 15, 2026, matokeo yataonesha sio tu aliyeshinda, lakini ni mikakati gani ya kampeni iliyovutia zaidi kipindi cha kampeni.

Kwa wanasiasa, wachambuzi, na raia kwa ujumla, uchaguzi unatoa taswira ya jinsi gani kampeni zimesaidia katika demokrasia na ni jinsi gani kampeni zinavyobadilika nchini Uganda.

Gcotyelwa Jimlongo ni mtaalamu wa Kampeni za Kisiasa kutoka kituo cha Political Campaign Resource Hub,  kampuni tanzu ya Kituo cha Kimataifa cha Kampeni za Kisiasa kilichopo Johannesburg, Afrika Kusini.