| Swahili
UTURUKI
3 dk kusoma
Rais Erdogan: Uhusiano kati ya Uturuki na Azerbaijan umeimarika
Rais wa Uturuki, amesema nchi yake iko tayari kuandaa tena mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul, huku akionya dhidi ya uwezekano wa kuanzishwa upya kwa mashambulizi dhidi ya Iran.
Rais Erdogan: Uhusiano kati ya Uturuki na Azerbaijan umeimarika
Erdogan alizungumza na waandishi wa habari aliporudi kutoka Azerbaijan, akieleze kuwa Uturuki na Azerbaijan ni mataifa ndugu. / / َAA

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesisitiza kuwa uhusiano kati ya Uturuki na Azerbaijan ni imara, akisema juhudi zozote zinazolenga kuvuruga uhusiano huo hazitafanikiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu, alipokuwa akirejea kutoka Azerbaijan, Erdogan amezitaja Uturuki na Azerbaijan kuwa mataifa ndugu yanayounganishwa na historia ya pamoja, urafiki na mshikamano.

Amesema wanaojaribu kuleta mgawanyiko kati ya mataifa hayo mawili hawajaelewa undani wa uhusiano wao pamoja na upendo uliopo baina ya wananchi wa nchi hizo.

Akiashria mkutano wake na Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, Erdogan amesema alimsalimia kwa kumkumbatia kwa furaha, jambo alilolitaja kuwa ishara ya ukaribu na uimara wa uhusiano wao.

Uturuki iko tayari kuandaa mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul

Akizungumzia vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, Erdogan amesema Uturuki inaendelea na juhudi kubwa za kidiplomasia zinazolenga kumaliza kabisa mzozo huo.

Ameeleza kuunga mkono juhudi za Rais wa Marekani, Donald Trump, za kuleta amani, akisema Uturuki inaunga mkono mipango inayolenga kusitisha vita hivyo.

Aidha, Erdogan amesisitiza kuwa Uturuki iko tayari kuwa mwenyeji wa duru nyingine ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul, akieleza matumaini yake kuwa juhudi za kidiplomasia zitazaa matunda na kuwezesha kupatikana kwa suluhu ya amani.

Erdogan aonya dhidi ya mashambulizi mapya dhidi ya Iran

Akizungumzia hali ya usalama katika eneo hilo, Erdogan amesema Uturuki haitaki kuona wimbi jingine la mashambulizi dhidi ya Iran wala kuendelea kuzorota kwa hali ya utulivu katika eneo zima.

Amsisitiza kuwa Uturuki inapinga hatua na matukio yanayoweza kuchochea upya uhasama na kuongeza hali ya kutokuwa na utulivu katika ukanda huo.

Ajenda ya COP31 inaweka suala la tabianchi kipaumbele

Akizungumzia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP31, ulioanza Jumatatu mjini Antalya, Erdogan ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti za kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Amesema: “Dunia ni makazi yetu sote, na hatuna haki ya kuichafua. Hapa Antalya, tutajadili hatua madhubuti za kuhakikisha mustakabali wa pamoja wa binadamu.”

Erdogan amesema Uturuki inaipa umuhimu maalum suala la mabadiliko ya tabianchi, akiongeza kuwa mkutano huo utazingatia ukuaji wa viwanda vya kijani, kujenga miji imara inayoweza kukabiliana na changamoto za tabianchi, kuongeza uelewa wa umaa na kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Erdogan athibitisha msimamo wa Uturuki kuhusu Cyprus

Kuhusu suala la Cyprus, Erdogan amesisitiza tena msimamo wa Uturuki kwamba kisiwa hicho kina makundi mawili tofauti ya watu na mataifa mawili tofauti.

Amesema: “Msimamo wetu kuhusu Cyprus uko wazi kabisa. Wakati umefika wa kukubali ukweli kwamba katika kisiwa hicho kuna jamii mbili tofauti na mataifa mawili tofauti.”

 

CHANZO:TRT World and Agencies