Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran “inaporomoka kabisa” huku uhasama kati ya Marekani na Irana ukiendelea.
Trump ameandika Jumatatu kwenye mtandao wake wa Truth Social, bila kutoa maelezo zaidi. Kauli hiyo inaendana na matamshi yake ya awali kuhusu hali ya kiuchumi na kijeshi ya Iran.
Siku ya umapili, Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, amesema Marekani ilikuwa ikiingia katika ‘hatua ya mwisho ya vita vya kiuchumi’ dhidi ya Iran, kufuatia kile alichodai kuwa ni hatua za utawala wa Trump za kusambaratisha uwezo wa kijeshi na nyuklia wa Iran.”
“Rais (Donald) Trump ameudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran, ameharibu karibu asilimia 100 ya viwanda vyake vya kijeshi, na amezika mpango wake wa nyuklia,” Bessent alisema katika chapisho kwenye mtandao wa X.
Ijumaa, Trump alisema bado anaamini Iran haikuwa tayari kufanya “makubaliano sahihi” na Marekani, wakati Marekani ikiendelea kuimarisha hatua za kiuchumi dhidi ya Iran.
“Wanatamani sana kufanya makubaliano, lakini kwa maoni yangu, hawako tayari kufanya makubaliano sahihi,” Trump aliwaambia waandishi wa habari.
“Hawana fedha, hawana jeshi la wanamaji, hawana jeshi la anga, hawawalipi wanajeshi wao, hawawalipi polisi wao. Wana mfumuko wa bei wa asilimia 350,” aliongeza.
Hapo awali Trump pia alidai kuwa Marekani inaendelea kuwa na “udhibiti kamili” wa eneo linalozunguka Mlango-Bahari wa Hormuz, pamoja na ardhi inayolizunguka kusini mwa Iran.
Marekani na Iran zilitia saini hati ya makubaliano ya uelewano mwezi Juni, iliyolenga kusitisha uhasama na kurejesha usafirishaji wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Hata hivyo, makubaliano hayo yalivunjika baadaye kutokana na kutokubaliana kuhusu namna ya kutekelezwa kwake na mustakabali wa usafiri wa majini kupitia njia hiyo muhimu.
Mzozo huo ulianza mwishoni mwa Februari baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran.
Iran ilijibu kwa kushambulia maeneo ya Israel pamoja na vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.














