Utajiri wa Afrika: Kaftan ya Morocco
Kaftan ni vazi mashuhuri nchini Morocco/ picha: UNESCO / Public domain
Utajiri wa Afrika: Kaftan ya Morocco
Kaftan huvaliwa wakati wa sherehe muhimu za kijamii na kidini kama vile harusi, ubatizo, matambiko ya wazee na sherehe nyengine.

Ikiwa umewahi kuvaa au kuona nguo maarufu kama kaftan ya Morrocan, basi bila shaka utakuwa unajua uzuri wa vazi hilo ambalo huwekwa katika kanzu au nguo ndefu zinazovaliwa na watu wa jinsia zote na umri katika matukio maalum na sherehe.

Mwaka 2025, UNESCO iliiorodhesha kaftan ya Morocco kama moja wapo ya Urithi muhimu wa Kitamaduni.

Kaftan inakuja kwa mitindo tofauti wa vitambaa na inaweza kuvaliwa bila mkanda wa mapambo.

Kutokana na asili mbalimbali za kitamaduni, vazi la kitamaduni linajulikana kwa kuweza kufunguka sehemu ya kati, vifungo na mapambo ya kuvutia, yaliyotengezwa kwa mikono, mara nyingi ikiwa ni pamoja na nyuzi za urembo, shanga na mapambo yanavyong'aa.

Utengezaji wa kaftan unafanywa tu na mafundi wenye ujuzi, ikiwa ni pamoja na wafumaji wanaozalisha vitambaa aina tofauti, washonaji wanaotengeneza vazi lenyewe, na mafundi wanaotengeza vifungo na mapambo.

Ujuzi unaohusiana na vazi hilo hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi chengine ndani ya familia na kupitia mafunzo yanayotolewa katika warsha maalum.

Watu wengine hujifunza kupitia elimu rasmi katika vituo vya mafunzo na shule za mitindo.

Kaftan, mbali na kuwa ni mavazi mazuri yanayoonesha utamaduni, lakini pia ni alama ya kijamii inayoonesha utajiri wa ubunifu.

Pia ni chanzo cha mapato kwa watu wengi wanaohusika katika uzalishaji na uuzaji wake. Hivyo basi, siku utakayokuwa nchini Morocco moja ya vitu ambavyo lazima ujipatie ni vazi la caftan.

CHANZO:TRT Swahili