TikTok imeanza kuwaomba waandaaji maudhui nchini Kenya kuwasilisha taarifa zao za mapato na makazi, katika hatua ya utekelezaji wa makato ya kodi.
Kwa mujibu wa viwango vilivyoripotiwa, wakazi wa Kenya wanaweza kukatwa asilimia 5, huku wasio wakazi wakikabiliwa na makato ya asilimia 20.
Hata hivyo, TikTok bado haijaweka wazi ni lini hasa utaratibu huo utaanza au namna viwango hivyo vitakavyotumika kwa aina mbalimbali za malipo wanayopokea watayarishaji maudhui.
Kwa hatua hiyo, TikTok inaungana na majukwaa mengine makubwa, yakiwemo Google, YouTube na Meta, ambayo tayari yanakata kodi katika mapato ya waandaaji wa maudhui.
Mabadiliko haya hayaishii kwenye kiasi cha fedha ambacho waandaaji maudhui watapokea. Pia yanaashiria mabadiliko katika namna kodi inayotokana na kazi za kidijitali inavyokusanywa, huku majukwaa yenyewe yakichukua nafasi kubwa zaidi katika mchakato huo.
Miongoni mwa taarifa zinazohitajika ni jina, anwani ya barua pepe, anwani ya makazi, nchi ya makazi. Hata hivyo, inaripotiwa kuwa kutoa anwani ya makazi ni jambo la hiari.
























