Mke wa Rais wa Uturuki atoa wito wa mtazamo mapya wa kimataifa ili kuboresha taasisi ya familia
Emine Erdogan ametaja changamoto zinazoibuka katika masuala ya idadi ya watu na kutoa wito wa sera za kimataifa zinazoweka familia katikati ya maendeleo ya kijamii.
Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan, ameitaka jumuiya ya kimataifa kubuni mtazamo mpya wa kuimarisha taasisi ya familia, akionya kwamba viwango vinavyoshuka vya uzazi na kuongezek kwa idadi ya wazee vinazisukuma jamii kuelekea “enzi ya kuporomoka kwa taasisi ya familia.”
Kupitia ujumbe wa video alioutuma kwa mkutano wa kimataifa wa “Growing Europe 2025” siku ya Jumanne, Erdogan alisema kuwa maisha ya kitamaduni ya kifamilia—pamoja na familia pana, sherehe za pamoja, na vizazi kukusanyika mezani kwa ushirika—yamepotea kwa kiasi kikubwa katika jamii za kisasa.
Alisema kuwa mabadiliko haya si ya kitamaduni pekee bali ni ishara za awali za dunia inayojitenga na kiini cha muundo wake wa kijamii.
Mke huyo wa rais alizungumzia mwenendo wa idadi ya watu duniani, akibainisha kuwa kiwango cha uzazi kimeshuka hadi wastani wa watoto 2.2 kwa kila mwanamke, na kwamba zaidi ya nusu ya nchi ziko chini ya kiwango kinachohitajika kubadili kizazi.
Kufikia mwaka 2030, mtu mmoja kati ya sita atakuwa na umri wa zaidi ya miaka 60, na idadi ya watu wenye miaka 80 na kuendelea inatarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo 2050.
“Kila kuzaliwa kw mtoto kunaleta siku mpya katika masika ya dunia,” alisema. “Kupungua kwa kiwango cha uzazi na kupungua kwa idadi ya vijana kunapunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuweka mzigo mkubwa wa kifedha kwenye mifumo ya hifadhi ya jamii na huduma za afya. Kwa kifupi, dunia isiyoweza kujirekebisha italazimika kukumbana na mgogoro mkubwa.”
Mwaka wa Familia
Aliangazia hatua ambazo Uturuki imechukua kukabiliana na changamoto hizi, ikiwemo kutangaza mwaka 2025 kuwa Mwaka wa Familia na kipindi cha 2026–2035 kuwa Muongo wa Familia na Idadi ya Watu.
Alisema kuwa sera kama vile mikopo ya nyumba na ndoa, likizo ya wazazi iliyoongezwa, msaada wa malezi ya watoto, na mipango ya kazi inayowapa wazazi unafuu, zinakusudia kupunguza mgongano kati ya majukumu ya kazi na maisha ya familia.
Erdogan pia alikosoa mitazamo ya kitamaduni inayoonyesha maisha ya familia kama kikwazo cha kufikia malengo binafsi, akisema kwamba “sekta ya utamaduni” ya kisasa inakuza sana ubinafsi huku ikipuuza familia.
Alieleza tumaini kwamba mkutano huo utakuwa jukwaa la kukabiliana na mitazamo hiyo na kuchochea ahadi madhubuti zaidi katika sera zinazolenga familia.
“Hatua tunazochukua kuiweka familia katikati ya jamii zitaleta pumzi mpya kwa dunia inayokua na uzee na upweke,” aliongeza.