Utajiri wa Afrika: Uganda kujenga upya utajiri wa faru
Faru wa kwanza wawili wamepelekwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kidepo / AP
Utajiri wa Afrika: Uganda kujenga upya utajiri wa faru
Faru wawili weupe wa kusini walihamishwa wiki iliyopita kutoka ranchi binafsi, na kuwa wanyama wa kwanza kati ya wanane waliopangwa katika kuishi katika mbuga hiyo.
tokea masaa 8

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 40, faru wamerudi katika Mbuga ya Taifa ya Kidepo Valley nchini Uganda.

Hii ni baada ya uwindaji haramu uliofanyika miaka ya nyuma na kusababishwa wote kuwindwa kwa ajili ya nyama na pembe zao zenye thamani.

Faru wawili weupe wa kusini walihamishwa wiki iliyopita kutoka ranchi binafsi, na kuwa wanyama wa kwanza kati ya wanane waliopangwa katika kuishi katika mbuga hiyo.

Faru wa mwisho katika mbuga hiyo aliuawa mwaka 1983.

Uganda ilikuwa ni makazi ya aina zote mbili za faru weusi na weupe wa kaskazini.

Kukosekana kwa hali ya utulivu nchini Uganda kumechangia idadi kubwa ya faru kuawa katika mbuga ya Kidepo na mbuga nyingine za Taifa za nchi hiyo.

Kulikuwa na takriban faru 700 katika mbuga hizo.

Ama katika nchi jirani ya Kenya, ambayo inawekeza zaidi katika uhifadhi, maisha ya faru yanaonekana kuwa na ahueni kiasi ambapo kuna zaidi ya faru weusi 1000 mashariki mwa nchi.

Kwa upande mwingine, Tanzania inaonesha mwelekeo mzuri katika idadi yake ya faru weusi, ambapo imeongezeka kutoka faru 190 mwaka 2020 hadi zaidi ya 260 mwaka 2024, kasi hii inatarajiwa kuongezeka.

Faru mweupe sasa analetwa nchini humo kupitia mpango mkubwa ulioanzwa Machi 2025.  Lengo ni kuleta faru weupe 36 kutoka Afrika Kusini hadi Bonde la Ngorongoro ili kuongeza tofauti za kijeni na idadi ya faru.

Kutokana na kasi hii ya ukuaji wa idadi ya faru katika nchi za Afrika Mashariki, ndio maana Uganda nayo sasa imepania kufufua utajiri wake faru.

Faru 8 wa kwanza walioletwa katika urithi wa asili wa mbuga ya Kidepo, eneo kubwa la savanna kaskazini mashariki mwa Uganda, wanaletwa kutoka ranchi binafsi ya Rhino Lake huko Nakasongola, takriban kilomita 100 kaskazini mwa mji mkuu wa Kampala.

Ranchi hiyo imekuwa ikizalisha faru tangu 2005.

Lakini jitihada hizi zinaweza kurudishwa nyuma na uwindaji haramu unasalia kuwa tatizo katika maeneo ya hifadhi ya wanyamapori nchini Uganda.

Ingawa mamlaka mara kwa mara zinakabiliana na majangili na kuwafunguliwa mashtaka, changamoto kubwa ni kuongezeka kwa mahitaji ya pembe za faru, kutokana na matumizi yao katika kutengeneza dawa za jadi na mapambo.

Mbuga ya Taifa ya Kidepo nchini Uganda, pia iko hatarini zaidi kwa sababu iko katika eneo ambalo wezi wa mifugo wenye silaha huvamia mara kwa mara kwa kuvuka mpaka. Hifadhi hiyo pia inapakana na Sudan Kusini, ambako serikali inapambana na ukosefu wa usalama.

CHANZO:TRT Swahili