ECOWAS yaiondolea vikwazo Guinea

Jumuiya hiyo iliiwekea Guinea vikwazo kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021.

By
Uamuzi wa ECOWAS, unafuatia kikao cha wakuu wa nchi za jumuiya hiyo, uliofanyika jijini Freetown, nchini Sierra Leone./Picha:ECOWAS

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imeiondolea vikwazo Guinea, kufuatia mapinduzi ya mwaka 2021.

Uamuzi wa ECOWAS, unafuatia kikao cha wakuu wa nchi za jumuiya hiyo, uliofanyika jijini Freetown, nchini Sierra Leone.

Kulingana na ECOWAS, uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Guinea mwezi Disemba mwaka jana, na makabidhiano halali ya madaraka kwa Rais Mamadi Doumbouya, yaliweka mazingira rafiki ya kurejesha utawala wa sheria nchini humo.

“Vikwazo vyote dhidi ya Jamhuri ya Guinea vimeondolewa kuanzia sasa,” ilisomeka taarifa iliyotiwa saini na Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Mwaka 2021, Jumuiya hiyo iliiwekea Guinea vikwazo kufuatia mapinduzi ya kijeshi.

Hata hivyo, katika taarifa yake, ECOWAS imesisitiza kuwa vikwazo hivyo havina umuhimu tena, kufuatia uchaguzi uliofanyika kwa mafanikio nchini humo.