Kaka wa Princes Diana, ‘amemshukia’ Mfalme Charles III wa Uingereza, akimhutuhumu kufurahia kifo cha dada yake.
Kupitia kitabu chake kipya, Charles Spencer anadai kuwa, Mfalme Charles III, alikuwa ni mtu mwenye furaha, usiku wa ajali iliyochukua uhai wa Diana, ambaye aliwahi kuwa mke wake.
Spencer alifananisha furaha ya Charles, kama ya mtu aliyetoka kushinda bahati nasibu, muda mfupi baada ya kutokea kwa ajali hiyo, Agosti 31, 1997.
Katika sehemu nyingine ya kitabu hicho, kilichochapishwa kwenye gazeti la Daily Mail siku ya Alhamisi, Spencer alidai kuwa, Charles atamsahau Diana, “muda mfupi tu baada ya kifo chake”.
Hata hivyo, kasri la Buckingham, limekana madai yaliyochapishwa kwenye gazeti hilo, huku magazeti mengi ya Uingereza yakiangazia majibizano kati Spencer na Mfalme Charles III.
"Mfalme anatambua maumivu anayopitia Charles kama kaka wa marehemu na namna machungu hayo yanavyoweza kuathiri namna ya kawaida ya mtu kufikiri," alisema msemaji wa kasri la Buckingham.
Sehemu ya kitabu hicho, kiitwacho "Swan Song: Diana, My Sister", kimechapishwa na gazeti la Daily Mail, la nchini Uingereza.
Ndani ya kitabu hicho, Spencer anadai kuwa, baadhi ya watu ndani ya kasri la Buckingham, walifurahia kifo cha Diana, huku akimtuhumu Charles kwa kusema uongo kuwa, watoto wake, William na Harry, wasingekuwa tayari kuwepo kwenye msafara wa mazishi.
Princess Diana alifariki dunia tarehe 31 Agosti 1997 kufuatia ajali mbaya ya gari mjini Paris, Ufaransa.
Ajali hiyo, iliyotokea ndani ya handaki la Pont de l'Alma, pia lilichukua uhai wa aliyekuwa mpenzi wa Diana, Dodi Al-Fayed, na dereva wao Henri Paul.





















