Serikali ya Mali imetoa maelezo kuhusu namna Waziri wa Ulinzi Sadio Camara alivyouawa, ikisema alifariki kutokana na majeraha aliyopata wakati wa makabiliano na magaidi waliomvamia nyumbani kwake.
Katika taarifa rasmi iliosomwa kupitia televisheni ya taifa Waziri wa Serikali za Mitaa, Brigedia Jenerali Issa Ousmane Coulibaly, ambaye pia ni msemaji wa serikali, anasema serikali ya mpito ilieleza kuwa mshambuliaji wa kujilipua alikuwa anaendesha gari na kuingia katika nyumba ya waziri eneo la Kati, mji muhimu wa kijeshi karibu na mji mkuu Bamako.
Inasemekana Camara alifyatuliana risasi na kufanikiwa ‘‘kuwakata makali’’ baadhi yao kabla ya yeye kupata majeraha mabaya. Alipelekwa hospitali, ambapo baadaye alifariki kutokana na majeraha.
Serikali imeongeza kuwa kuporomoka kwa nyumba ya waziri kulisababisha watu wengine zaidi kufariki na pia kuharibu msikiti uliokuwepo karibu, kusababisha waumini waliokuwepo kufariki dunia.
“Ni matukio ya kuhuzunisha, Jenerali Assimi Goita, rais wa mpito, mkuu wa nchi na kamanda mkuu wa majeshi, serikali na watu wa Mali, wanatuma salamu zao za rambirambi kwa familia ya waziri huyo,” taarifa ilisema.
Salamu za rambirambi pia zilitolewa kwa raia wote waliouawa pamoja na wanajeshi katika mashambulizi ya Aprili 25.
Utaratibu wa asubuhi
Wale walioshuhudia, ambao hawakutaka kutajwa wanasema huenda waziri alikuwa anaendelea na utaratibu wake wa asubuhi wakati wa mashambulizi hayo.
“Huwa anafanya mazoezi mapema, na baada ya hapo, huwa anaenda kwenye msikiti ulio karibu na nyumba yake kwa swala ya alfajiri,” mkazi mmoja alisema.
Haijulikana kama alikuwa nyumbani kwake au alikuwa anaenda msikitini wakati wa mashambulizi hayo.
Mashambulizi hayo yalitokea kama sehemu ya mashambulizi yaliyolenga maeneo ya kimkakati ya jeshi kote nchini Mali. Jeshi linasema operesheni zinaendelea mjini Bamako, Kati na maeneo mengine kuwasaka waliohusika, likiongeza kuwa magaidi wengi “wamekatwa makali.”
Mji wa Kati, uko karibu kilomita 15 kutoka mji wa Bamako, ni moja ya ngome muhimu ya kijeshi na kihistoria na umekuwa msingi wa siasa za Mali na Usalama.
Mwanajeshi Camara
Camara alizaliwa 1979, amekuwa mwanajeshi ambaye alipanda vyeo katika jeshi la Mali. Alipata baadhi ya mafunzo yake ya kijeshi nchini Urusi.
Alipata umaarufu kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya 2020 yaliyomuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita na kuteuliwa waziri wa ulinzi kipindi cha mpito. Aliteuliwa tena baada ya 2021 wakati jeshi lilipofanya mapinduzi mengine na kuingia madarakani Assimi Goita.
Akiwa waziri wa ulinzi, Camara alionekana kama mtu muhimu kwa masuala ya kimkakati na kiusalama dhidi ya makundi yenye silaha, pamoja na kusimamia mabadiliko jeshini na misimamo ya ushirikiano kimataifa. Wakati akiwa waziri ndipo vikosi vya kigeni vilipoondoka nchini, ikiwemo wanajeshi wa Ufaransa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa.
Mkuu wa Majeshi wa Mali Jenerali Oumar Diarra amesema katika televisheni ya taifa kuwa magaidi walifanya mashambulizi zaidi ya 20 kote nchini.
Alisema vikosi vya Mali vimewakata makali magaidi zaidi ya 200 na kupata silaha nyingi.
Raia waombwa kuwa watulivu
Diarra alieleza kuwa sasa hivi magaidi wanavaa sare za jeshi ili kujichanganya na raia na kununua bidhaa karibu na miji na vijiji.
Anasema katika eneo la Kidal, wanajeshi wa Mali wamekuwa wakijipanga hasa katika kijiji cha Anefis.
Diarra aliongeza kuwa lengo kubwa la magaidi ni kusababisha hali ya kutokuwa na usalama nchini.
Katika ujumbe kwa watu, aliwaomba raia kuwa watulivu na kutoa nafasi kwa vikosi vya ulinzi na usalama kufanya kazi yao.
Alionya kuhusu kusambaza uvumi na taarifa potofu, akiwashauri kuwa taarifa za kweli zitatoka jeshini tu. Pia aliwataka watu kutoa taarifa kwa maafisa wa usalama pale wanapoona vitendo vya kutilia shaka.













