Wafahamu baadhi ya ndugu na mapacha waliowahi kucheza pamoja michuano ya AFCON

Imekuwa ni jambo la kawaida kushuhudia mapacha na ndugu wa familia moja, kuchezea mataifa yao kwa pamoja, wakati wa michuano ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika, maarufu kama AFCON.

By Edward Josaphat Qorro
Kolo na Yaya Toure wamekuwa ni sehemu ya mafanikio ya timu ya taifa ya Ivory Coast./Picha: @SI_FootballClub

Wakati michuano ya AFCON 2025 ikianza wikiendi hii nchini Morocco, je unawafahamu baadhi ya ndugu na mapacha waliowahi kuchezea timu zao za taifa kwenye mashindano hayo?

Ndugu wawili kutoka familia ya Toure; nawazungumzia Kolo na mdogo wake Yaya, waliwasaidia Tembo wa Ivory Coast kufika fainali ya AFCON mwaka 2006, 2012 na kutwaa kombe hilo mwaka 2015 nchini Equatorial Guinea.

Ndugu hao wawili wameshiriki jumla ya michuano sita ya AFCON wakiwa na timu ya taifa ya Ivory Coast.

Nadhani unamkumbuka Abedi Pele, yule gwiji wa soka kutoka Ghana.

Abedi Ayew Pele, alikuwa na watoto watatu; Andre, Ibrahim pamoja na Jordan Ayew ambao waliiwakilisha Ghana kwenye michuano ya AFCON.

Kwa miaka 13, Andre Ayew na ndugu yake Jordan, wameiwakilisha Black Stars ya Ghana kwenye michuano ya AFCON, licha ya kutobeba kombe hilo.

Ndugu hao wanakumbukwa zaidi kwa ushirikiano wao uwanjani, hasa wakati wa fainali za mwaka 2012 zilizofanyika Equatorial Guinea na Gabon, ambapo Ghana ilipoteza kwa Zambia kwenye hatua nusu fainali.

Kabla ya hapo, waliwahi pia kucheza pamoja na ndugu yao aitwaye Ibrahim Ayew, kwenye AFCON ya mwaka 2010.

Wakijulikana kwa muonekano wa vipara vyao ving’aavyo, Ibrahim Hassan na pacha wake walijipatia umaarufu mkubwa, wakati wakiwachezea mafarao wa Misri.

Wakati Hossam akikumbukwa kuwa uhodari wake wa kufunga magoli, Ibrahim alijulikana zaidi katika nafasi ya ulinzi.

Mapacha hao wameshinda mataji ya AFCON mara mbili katika maisha yao ya soka, kabla ya kutundika daluga.

Huwezi kuzungumzia mafanikio ya timu ya taifa ya Zambia, maarufu kama ‘Chipolopolo’, bila kumtaja Felix na ndugu yake Christopher Katongo.

Ndugu hao wawili, mmoja akichezea nafasi ya kiungo huku mwingine akiwa idara ya ushambuliaji, wameshiriki michuano ya AFCON mara tano, kati ya mwaka 2006 na 2013.

Ndugu hao walilishangaza bara la Afrika baada ya kuisaidia Zambia kutwaa kombe la AFCON mwaka 2012, katika fainali zilizofanyika Equatorial Guinea na Gabon.

Mwaka 1994, timu ya taifa ya Zambia, ilifanikiwa kufika fainali ya michuano ya AFCON nchini Tunisia kabla ya kufungwa na Super ya Eagles ya Nigeria kwa mabao 2-1.

Wakiiwakilisha timu ya taifa ya Zambia, nahodha Kalusha Bwalya alikuwa na mdogo wake Joel Bwalya wakati Kenneth Malitoli alicheza na kaka yake Mordon Malitoli kwenye fainali hizo za Tunisia.

Wengine ni pamoja na Francois Omam-Biyik na ndugu yake Andre Kana-Biyik, walioiwakilisha Cameroon, Solomon Kalou na Bonaventure Kalou wa Ivory Coast.

Pia wapo Laryea Kingston na Richard Kingston waliowahi kuichezea Black Stars ya Ghana.