Rais wa Marekani, Donal Trump, ameondoa wazo la kutoza ada ya asilimia 20 kwa mizigo yote inayosafirishwa kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz, na badala yake amesema atazingatia mikataba ya biashara na uwekezaji pamoja na nchi za Ghuba.
Mabadiliko hayo ya msimamo yanajiri siku moja baada ya Trump kupendekeza kutoza ada hiyo ya asilimia 20 kwa lengo la kulinda njia hiyo muhimu ya majini.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa Truth Social siku ya Jumanne, Trump alisema: "Kutokana na mazungumzo yenye tija na viongozi wa Mashariki ya Kati, nimeamua kuachana na mpango wa ada ya asilimia 20 na badala yake kufanya mikataba ya biashara na uwekezaji na nchi za Ghuba."
Hata hivyo, Trump hakutaja ahadi zozote maalumu zilizotolewa na nchi za Ghuba, akisema tu kuwa uwekezaji huo "utakuwa mkubwa sana, lakini wakati huohuo utakuwa na manufaa makubwa kwao na kwa mustakabali wao."
Muda mfupi baada ya Trump kutoa pendekezo la ada hiyo ya asilimia 20 siku ya Jumatatu, shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya usafirishaji wa majini lilisema linapinga kutozwa kwa ada kwa meli zinazopita katika njia za maji za kimataifa. Hata hivyo, shirika hilo lilisema litasubiri maelezo zaidi kuhusu mpango huo wa Trump.
Katika ujumbe wake siku ya Jumanne, Trump alisisitiza kuwa Mlango wa Hormuz uko wazi kwa meli zote isipokuwa meli za Iran.
Alisema: "Kwa hiyo tutakuwa na kizuizi, lakini ni kwa meli zinazoingia au kutoka katika bandari za Iran, au zinazobeba chochote kinachohusiana na mizigo ya Iran."
















