Uwanja wa Ndege wa Ankara katika mji mkuu wa Uturuki ulifunguliwa siku ya Jumatatu kabla ya mkutano wa viongozi wa NATO unaotarajiwa kufanyika katika jiji hilo Julai 7-8, huku Rais Recep Tayyip Erdogan akisema njia za sasa za usafiri zitasaidia wajumbe watakaowasili kufika katika eneo la mkutano.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi ya Uwanja wa Ndege wa Ankara, Erdogan alisema miradi hiyo itaimarisha miundombinu ya safari za anga na usafiri jijini Ankara wakati mji huo mkuu ukijiandaa kwa kongamano la Julai 7-8.
“Kwa barabara ya kilomita 3-ambayo kuna sehemu iliyogawanywa, tutaunganisha moja kwa moja ili wajumbe wapate kufikia Kongamano la NATO kwa urahisi,” alisema.
Huu ni uwanja wa ndege wa pili katika mji mkuu, mwingine ni Uwanja wa Ndege wa Esenboga, ambao unatoa huduma kwa safari za ndani na za kimataifa.
Erdogan anasema ujenzi wa uwanja huo wa ndege na uwekezaji mwingine ulikamilika kwa “haraka zaidi’’ ndani ya siku 230, akiongeza kuwa barabara ya kilomita 12.5 imejengwa, ikiwemo kilomita 6.5 ya pande kadhaa za barabara na kilomita 6 ya barabara moja.
Amesema miradi hiyo imesaidia kuwepo kwa mtandao imara wa usafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Ankara hadi katikati mwa mji ikiwa ni zaidi ya kilomita 17.
Uturuki inakuwa kituo cha diplomasia ya kimataifa
Rais anasema nafasi ya Ankara katika masuala ya diplomasia inaimarika kila mwaka wakati uwezo wa Uturuki katika siasa za dunia ukiongezeka.
“Uturuki, ambayo inaungana na nchi 67 zenye idadi ya watu bilioni 1.5 ambazo safari zake za ndege ni saa nne tu, sasa imeanza kuwa kituo cha diplomasia ya kimataifa, ikiwa na miji ya Ankara, Istanbul na Antalya,” amesema.
Erdogan pia alieleza kuwa hafla nyingi za kimataifa ambazo Uturuki ni wenyeji 2026, ikiwemo Jukwaa la Taka Sifuri, ambalo lilifanyika jijini Istanbul Juni 5-7 na kuwaleta pamoja washiriki zaidi ya 5,000 kutoka nchi 183.
Alisema Uturuki itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la 77 kuhusu Masuala ya Anga mwezi Oktoba, kisha Mkutano wa 13 wa Mataifa yanayozungumza Kituruki na kongamano la COP31 kuhusu tabianchi mwezi Novemba.
Uwanja wa Ndege umeandaliwa kwa ajili ya ndege kubwa, ndege rasmi
“Pamoja na Uwanja wa Ndege wa Ankara, siyo tu tumeleta mradi mpya katika mji wetu mkuu. Tumefufua mradi ambao utakuwa na athari kubwa kwa historia yetu ya safari za anga,” Erdogan anasema.
Anasema uwanja huo wa ndege, uliojengwa 1933 kwa maagizo ya baba wa taifa wa jamhuri Gazi Mustafa Kemal Ataturk, na kwa muda mrefu ukitumika kama ngome ya masuala ya anga ya kijeshi, umejengwa kwa muonekano mpya na maeneo kuimarishwa.
Sehemu ya kupaa na kutua kwa ndege iliongezwa kutoka mita 2,450 hadi mita 3,000 kwa urefu, huku upana ukiongezwa kutoka mita 42 hadi mita 60, na maeneo yake yote mengine kujengwa upya, Erdogan amesema.
Sehemu mbili za kugeuka ndege ambazo ni mita mraba 15,000 zimejengwa katika pande zote mbili za uwanja huo, ilhali sehemu mpya ya kuegesha ndege ya mita mraba 160,000 iliongezwa, kuruhusu ndege 44 kuegeshwa bila tatizo kwa wakati mmoja, alisema.
Erdogan anasema mifumo ya taa, taa za maeneo ya kutua, na za kuongoza sehemu za kupaa ni za kisasa zaidi kulingana na viwango vya kimataifa vya safari za anga.
Ikulu ndogo ya rais yenye ukubwa wa mita mraba 4,800 na yenye sehemu ya wazi ya kuegesha magari 310 pia ilijengwa katika uwanja huo wa ndege, aliongeza.
Erdogan anasema Uwanja wa Ndege wa Ankara una uwezo wa kupokea ndege kubwa pamoja na ndege rasmi, ikiwa na maeneo makubwa ya kutua na kupaa, sehemu ya kuegesha ndege, njia za kisasa, na miundombinu ilioimarishwa.
Daraja la urefu wa mita 140 la Baskent lilijengwa katika njia ya treni ya mwendokasi, amesema, akiongeza kuwa tani 10,000 za daraja hili ziliwekwa katika njia ambayo haijawahi kutumika hapo awali nchini Uturuki.
Esenboga uliwahi kuwa uwanja wa 4 Uturuki wenye abiria wengi wakati wa sikukuu
Wakati wa siku tisa za Sikukuu, viwanja vya ndege vya Uturuki vilikuwa na safari za ndege 51,962 na kuhudumia abiria milioni 7.6, Erdogan alisema.
Aliongeza kuwa Uwanja wa Ndege wa Esenboga ulikuwa wa nne nchini Uturuki kupokea abiria wengi zaidi wakati wa sikukuu hiyo, kukiwa na safari za ndege 2,557 na abiria 382,000.
Rais anasema Esenboga, ambayo ilikuwa ikihudumia abiria milioni 3 kila mwaka miaka 20 iliopita, sasa inahudumia abiria milioni 15 kila mwaka, akiongeza kuwa kufunguliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Ankara kutasaidia kupunguza msongamano uwanjani na katika barabara za karibu na Esenboga na njia ya uwanja wa ndege.
Ndege ya Erdogan ililakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Ankara kwa heshima ya maji yaliyotoka kwenye mabomba kabla ya hafla hiyo.
Baada ya dua, Erdogan alifungua rasmi Uwanja wa Ndege wa Ankara, Daraja la Baskent, na barabara zinazounganisha eneo hilo.

















