| Swahili
MICHEZO
2 dk kusoma
Cristiano Ronaldo atangaza azma yake ya kustaafu soka
Kauli za Ronaldo, ambaye mkataba wake na Al Nassr unaendelea hadi Juni 2027, zimekuja baada ya mpinzani wake wa muda mrefu, Lionel Messi, kueleza pia mashaka kuhusu kuendelea kucheza soka, kufuatia kifo cha baba yake Jorge, mwezi huu.
Cristiano Ronaldo atangaza azma yake ya kustaafu soka
Ronaldo alifunga mabao matatu katika Kombe la Dunia la 2026, huku Ureno ikifika hatua ya 16 bora. / / Reuters

Cristiano Ronaldo amesema huenda akaamua kustaafu soka baada ya mkataba wake na Al Nassr kumalizika msimu ujao, huku akisema anapanga kutumia muda mwingi zaidi “kufurahia maisha”.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41, amebakisha mabao 24 pekee kufikisha mabao 1,000, amesema kwamba hakuwa na mpango wa kuendelea kubaki kwenye soka na badala yake angependa kutumia muda zaidi na familia yake na kufuatilia heka heka zingine.

Nyota huyo wa timu ya taifa ya Ureno, anayetambuliwa kwa upana kuwa miongoni mwa wanasoka bora zaidi wa muda wote, ametoa kauli hizo baada ya kufunga ndoa na mwenza wake wa muda mrefu, Georgina Rodriguez, mapema mwezi huu.

“Huenda huu ukawa mwaka wangu wa mwisho katika soka, na nataka kuondoka nikiwa nimeacha urithi wa kuvutia sana,” Ronaldo alisema katika mahojiano na Vogue.

“Nimepanga tayari maisha yangu ya baadaye. Nina mambo mengi sana yatakayonishughulisha kiasi kwamba ni vigumu kukuambia jambo moja tu. Kwa sababu nikiwacha soka huenda nikawa na muda mwingi zaidi, hivyo unatakiwa kujaza muda wako kwa njia mbalimbali, si kwa jambo moja tu.

“Pia nataka kujifurahisha zaidi, kusafiri zaidi, kutazama na kucheza padeli (unaofanana na mchezo wa tenisi), mchezo ambao ninaoupenda sana, na kuendelea kufurahia kile nilichokipata—kile tulichokipata. Kwa sababu, baada ya yote, imekuwa miaka 25 yenye kujitolea na kujinyima mambo mengi.”

Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or alianza maisha yake ya soka la kulipwa miaka 24 iliyopita akiwa na Sporting CP ya Lisbon, Ureno. Baadaye alitumia miaka sita Manchester United, kabla ya kujiunga na Real Madrid ambako alicheza kwa misimu tisa na kufunga mabao 450 katika mechi 438.

Kisha Ronaldo alihamia Juventus akaichezea timu hiyo ya Italia kwa misimu mitatu, kabla ya kurudi Manchester United, na baadae kujiunga na klabu ya Al Nassr ya nchini Saudi Arabia, Januari 2023.

Kauli za Ronaldo, ambaye mkataba wake na Al Nassr unaendelea hadi Juni 2027, zimekuja baada ya mpinzani wake wa muda mrefu, Lionel Messi mwenye umri wa miaka 39, kuonesha wasiwasi wake kuhusu kuendelea na soka “kwa muda mrefu zaidi”, kufuatia kifo cha baba yake, Jorge Messi, mwezi huu.

Ronaldo alifunga mabao matatu katika Kombe la Dunia la 2026, huku Ureno ikifika hatua ya 16 bora. Kabla ya michuano hiyo kuanza, alithibitisha kwamba Kombe la Dunia la 2026 litakuwa la mwisho kwake kushiriki.

CHANZO:TRT Afrika