| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Luteni mstaafu wa Uganda kupelekwa Marekani kujibu tuhuma za kusafirisha silaha kwa magenge Mexico
Katungi Michael Mpeirwe, luteni mstaafu wa Jeshi la Uganda, anatuhumiwa kula njama ya kusambaza silaha zenye thamani ya takribani dola milioni 54 kwa magenge ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini Mexico.
Luteni mstaafu wa Uganda kupelekwa Marekani kujibu tuhuma za kusafirisha silaha kwa magenge Mexico
Ofisi ya Mashtaka ya Uganda ilisema imeidhinisha kupelekwa kwa Mpeirwe nchini Marekani. /ugandarn

Waendesha mashtaka nchini Uganda wamekubali Ijumaa kumpeleka nchini Marekani mwanajeshi huyo wa zamani wa Uganda, ambako anakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kusambaza silaha kwa magenge yanayohusishwa na dawa za kulevya nchini Mexico.

Mpeirwe, ambaye ni luteni mstaafu wa Jeshi la Uganda, anatuhumiwa kushiriki katika njama ya kusambaza silaha zenye thamani ya takribani Dola milioni 54 kwa magenge mbalimbali, likiwemo genge maarufu la Cartel de Jalisco Nueva Generacion (CJNG).

Ofisi ya Mashtaka ya Uganda ilisema imeidhinisha kupelekwa kwake nchini Marekani.

Hati ya mashtaka iliyowasilishwa katika jimbo la Virginia nchini Marekani inasema Mpeirwe anadaiwa kuwa sehemu ya njama ya kusafirisha kwa njia ya magendo bunduk, virushaji roketi, mabomu, vifaa vya kuona wakati wa usiku, bunduki za kufyatulia kwa usahihi kutoka umbali mrefu (sniper), mabomu ya ardhini, pamoja na silaha za kukabiliana na ndege.

Silaha hizo zilidaiwa kupelekwa kwa magenge ya dawa za kulevya, likiwemo CJNG, ambalo limeelezwa kuwa “moja ya mashirika ya uhalifu ya kimataifa yenye ukatili mkubwa na shughuli nyingi zaidi nchini Mexico.”

‘Makombora na ndege zisizo na rubani’

Hati ya mashtaka ilisema Mpeirwe alikuwa akishirikiana na mfanyabiashara wa silaha kutoka Bulgaria, Peter Dimitrov Mirchev, pamoja na raia mmoja wa Kenya na mmoja wa Tanzania, katika kusafirisha silaha hizo kutoka Bulgaria hadi Tanzania, na baadaye kuzipeleka kwa magenge hayo.

“Watuhumiwa wanadaiwa kuendelea kula njama ya kusambaza silaha zaidi kwa magenge na walanguzi wa dawa za kulevya, ambazo huenda zilijumuisha makombora ya kutoka ardhini kwenda angani, ndege zisizo na rubani za kushambulia ndege, pamoja na mfumo wa silaha za kukabiliana na ndege aina ya ZU-23,” hati hiyo ya mashtaka ilisema.

Mirchev aliwahi kutuhumiwa kuhusika katika kusambaza silaha kwa Viktor Bout, mfanyabiashara maarufu wa silaha kutoka Urusi ambaye alirejeshwa nchini Urusi mwaka 2022 kupitia makubaliano ya kubadilishana wafungwa na Marekani.

Mirchev alikamatwa nchini Hispania mwezi Aprili 2025 na kupelekwa nchini Marekani mapema mwaka huu.