Marekani ‘kupitia upya’ uhusiano wake na Tanzania
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inasema kuwa haiwezi kudharua matukio yenye kuhatarisha usalama wa raia wa Marekani waliopo nchini Tanzania
Marekani imesema kuwa unapitia upya uhusiano wake na nchi ya Tanzania, ikisema kuwa imeshtushwa na matukio ya hivi karibuni yaliyotokea nchini humo.
Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, nchi hiyo inaendelea kuthamini uhusiano wake na watu wa Tanzania, ambao umechangia pakubwa kwenye usalama wa kikanda na kukua kwa uchumi.
Hata hivyo, katika taarifa yake, Marekani imesisitiza kuwa haitoweza kudharau yale yanayoendelea nchini Tanzania, huku yakiyaweka maisha raia wa Marekani na biashara zake hatarini.
"Na ndio maana, Marekani inapitia kwa ukamilifu, uhusiano wake na serikali ya Tanzania," ilisema wizara hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Marekani imeshtushwa na ukandamizwaji wa haki ya mbalimbali, ikiwemo za kidini, uhuru wa maoni, vikwazo endelevu dhidi ya biashara za Kimarekani na mauaji ya raia wakati na baada ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
"Matukio haya yanahatarisha usalama wa raia wetu pamoja na maslahi ya nchi yetu na yanaweka rehani uhusiano wetu uliodumu kwa muda mrefu.
“Marekani haitodharau matukio haya yenye kuhatarisha usalama wa raia wetu, au usalama na utulivu wa kikanda," ilisema wizara hiyo.