Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mji wa kimkakati wa El-Obeid nchini Sudan huenda ukawa chini ya udhibiti wa wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) kutokana na vikosi vyao kukusanyika eneo hilo kwa kile maafisa wa misaada wanasema huenda ikawa mashambulizi makali.
Onyo hilo limezua wasiwasi kuwa El-Obeid, mji mkuu wa Jimbo la Kordofan Kaskazini, huenda ukakabiliwa na hatima kama ya Al Fasher huko Darfur, ambapo RSF iliudhibiti mji huo baada ya mapigano ya muda mrefu. Umoja wa Mataifa ulisema mashambulizi ya mwezi Oktoba huko Al Fasher yana ishara "za mauaji ya halaiki."
Kuwa wakazi karibu 500,000 na wengine takriban 100,000 wameondolewa katika makazi yao na mapigano hayo maeneo mengine ya Sudan, katika wiki za hivi karibuni El-Obeid umekabiliwa na mashambulizi mabaya ya RSF tangu kuanza kwa mapigano.
Mohamed Refaat wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji pia ameonya kuwa mji huo unakaribia kudhibitiwa kabisa, na raia "watashindwa kuondoka au kurudi".
Kama ilivyofanyika Al Fasher
Bila kuongeza misaada kwa watu, hali mjini El-Obeid inaweza kuwa kama Al Fasher "katika wiki" chache zijazo, ambapo raia walilazimika kula chakula cha wanyama katika kipindi cha miezi 18 ya mashambulizi, alisema.
Jeshi la Sudan lilifanikiwa kuwatimua RSF mji wa El-Obeid mwezi Februari mwaka uliopita na limejaribu kuzuia wapiganaji hao wasidhibiti eneo hilo.
Mashambulizi ya hivi karibuni ya RSF yamesababisha uharibifu katika kituo kikuu cha kufua umeme na visima vya mafuta, kufanya maeneo kuwa gizani na kutatiza usambazaji wa maji baada ya mabomba kushambuliwa.
El-Obeid ni sehemu ya kimkakati inayounganisha maeneo yanayodhibitiwa na jeshi ya kati na mashariki mwa Sudan, ikiwemo Khartoum.
Mji huo pia kuna kikosi cha askari wa jeshi, uwanja wa ndege wa jeshi, bomba muhimu la mafuta na moja ya sehemu kubwa ya biashara ya gundi Sudan.
Huku mapigano yakiendelea na watu kushindwa kufika eneo hilo, ni vigumu kupata taarifa za uhakika kutoka El-Obeid.
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa watu zaidi 6,000 waliuawa katika siku tatu za mwanzo wakati RSF ilipodhibiti El-Fasher, huku serikali za Magharibi zikionya kuwa ukatili kama huo unaweza kutokea iwapo El-Obeid itadhibitiwa.















