Mauritius yalaani shambulizi la Iran dhidi ya kisiwa chake cha Chagos, yataka diplomasia itumike

Mauritius imetaka kusitishwa haraka kwa mapigano kwa maslahi ya watu wa eneo hilo na utulivu wa dunia kwa ujumla.

By
Mauritius imelaani vikali kushambuliwa kwa kisiwa chake cha Chagos. / AP

Serikali ya Mauritius imeelezea wasiwasi wake kufuatia shambulizi la kombora lililolenga Kisiwa cha Chagos kati ya usiku wa kuamkia Alhamisi ya tarehe 19 Machi na Machi 20.

"Shambulizi hilo ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na linahatarisha amani na utulivu wa eneo la Bahari ya Hindi," imesema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.

Wakati huo huo, Mauritius imetaka kusitishwa haraka kwa mapigano kwa maslahi ya watu wa eneo hilo na utulivu wa dunia kwa ujumla.

Taarifa hiyo ya Machi 23, imetilia mkazo umuhimu wa mazungumzo na diplomasia katika kutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati ambao umeanza Machi 28 baada ya Marekani na Israel kufanya mashambulizi ya pamoja dhidi ya Iran, hivyo kuilazimu Iran kulipiza kisasi kuishambulia Israel na maeneo ya nchi za Ghuba yenye kambi za Marekani.

Mgogoro huo ambao umeingia wiki ya tatu tangu kuanza, tayari umeibua hofu kubwa katika uchumi wa dunia, hasa baada ya bei ya mafuta kupanda kutokana na agizo la Iran la kufunga Mlango Bahari wa Hormuz ambao ndio njia kuu ya usafirishaji wa mafuta na bidhaa nyengine.