Utajiri wa Afrika: Nyangumi wa Afrika Kusini

Nyangumi ni mamalia wa baharini wenye damu joto, miili yao iliyosawazishwa na safu ya mafuta kwa ajili ya joto, na kuundwa kwa njia ya kuwawezesha kujiendesha mbele na kuogelea kwa urahisi.

By Coletta Wanjohi
Nyangumi wa Afrika Kusini / Reuters

Je, unajua kwamba watu husafiri kutoka mbali hadi Afrika Kusini kutazama nyangumi?

Kuanzia Juni hadi Novemba maji ya Afrika Kusini haswa katika sehemu inayoitwa Hermanus, huwa ni kivutio cha aina tofauti za nyangumi.

Spishi zinazojulikana zaidi hapa ni Nyangumi wa Kusini, Humpback, na Bryde, ambao huhama kutoka Antaktika hadi hapa kujamiiana na kuzaa katika maji haya ya pwani yenye joto.

Hapa utapata nyangumi wenye urefu wa zaidi ya mita 15 na uzito wa kilo 80,000 au hata zaidi.

Vipindi vya ujauzito wa nyangumi kawaida huanzia miezi 10 hadi 18, kulingana na spishi.

Nyangumi kwa ujumla huzaa mtoto mmoja tu kwa wakati mmoja na kwa kawaida hufanya hivyo kila baada ya miaka 2-4, au wakati mwingine hadi kila baada ya miaka 10 kwa spishi zilizo hatarini kutoweka.

Nyangumi ni mamalia wa baharini wenye damu joto, miili yao iliyosawazishwa na safu ya mafuta kwa ajili ya joto, na kuundwa kwa njia ya kuwawezesha kujiendesha mbele na kuogelea kwa urahisi.

Wanakuja juu ya uso wa maji ili kupata hewa safi.

Wataalamu wanawaelezea kuwa ni viumbe wenye akili nyingi na pia wanaimba!

Nyangumi wa kiume ndio waimbaji wanaofahamika zaidi na nyimbo zinaweza kudumu kwa hadi dakika 30 na kujumuisha mada mbalimbali zinazoimbwa kwa mlolongo ambao ni wa kawaida kwa madume wote katika eneo moja la kuzaliana mwaka huo.

Baadhi ya aina ya nyangumi wana meno ambayo huyatumia kuwinda hasa samaki, ngisi na pweza.

Spishi nyingine hufungua midomo yao kwa upana na kumeza maji mingi ya baharini, ambapo mawindo yao hunaswa.

Kwa wastani, nyangumi huishi kati ya miaka 20 na 90. Walakini, spishi nyengine inasemekana zinaishi kwa zaidi ya miaka 200.

Wanyama hawa adimu hata hivyo wanakabiliwa na hatari. Maeneo makubwa, hasa nje ya pwani ya kusini mwa Afrika, ambayo njia kubwa za meli zenye zinazokatiza njia za uhamaji wa nyangumi, na husababisha majeraha mabaya.

Nyangumi mara nyingi hunaswa kwenye nyavu za wavuvi na uchafu wa baharini.

Wataalamu pia wanasema maji yanayoanza kuwa  joto katika Antaktika yanapunguza usambazaji wa chakula, na kusababisha nyangumi kufika katika mwambao wa Afrika wakiwa wamekonda na kuathiri uwezo wao wa kunyonyesha watoto wao.

Yote kwa yote ikiwa utawahi kujipata katika pwani ya Afrika Kusini, jitahidi kwenda kuwaangalia nyangumi na pengine unaweza kubahatika kuwasikia wakiimba.