Hukumu ya kifo ya Jospeh Kabila inavyotikisa diplomasia na siasa ndani na nje ya DRC
Waangalizi wengi wa kimataifa na DRC wanasema kesi hiyo ilikuwa na muelekeo wa wazi wa kisiasa hivyo kuibua maswali kuhusu utaratibu unaostahili na utekelezwaji wa vyombo vya mahakama.
Kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja, jina la Joseph Kabila lilitulia kimya ndani na nje ya DRC. Rais huyo wa zamani alijipeleka uhamishoni mwenyewe bila kujulikana kwa uhakika alikuwa wapi au alikuwa anafanya nini.
Lakini kufikia mwezi Aprili 2025, mara alianza kusikika akichangia siasa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kufikia mwezi Mei, akatikisa siasa za nchi hiyo kwa kurejea nchini, japo Mashariki mwa nchi ambako anadaiwa kuwa na uungwaji mkono au ushawishi na makundi ya waasi yanayopigana na serikali.
Katika kesi inayoonekana kuharakishwa, Mahakama ya kijeshi ilimtia hatiani Kabila bila kuwepo kwa uhalifu mkubwa - ikiwa ni pamoja na uhaini na uhalifu wa kivita na kumpa hukumu ya kifo - kuhusiana na madai ya kushirikiana na waasi wa M23 ambao walienea katika maeneo ya Kivu Kaskazini na Kusini mapema mwaka huu.
Mahakama pia ilimuamuru Kabila kulipa fidia ya dola bilioni 29 kwa DRC, pamoja na dola bilioni 2 kwa jimbo la Kivu Kaskazini nchini humo na dola bilioni 2 kwa Kivu Kusini. Kabila amekana mashtaka hayo.
Hukumu hii inamaanisha nini ?
Waangalizi wengi wa kimataifa na DRC wanasema kesi hiyo ilikuwa na muelekeo wa wazi wa kisiasa na kuibua maswali kuhusu utaratibu unaostahili na utekelezwaji wa vyombo vya mahakama. Human Rights Watch ilisema kuwa kesi hiyo inaonekana kama kisasi kinachotishia athari kubwa kwa sheria ya nchi.
‘‘Hukumu iliyotolewa kwa rais Kabila kutokana na madai ya kuwa na uhusiano na M23 sio tu ni maonesho ya haki lakini pia ni ukiukaji mkubwa wa tamko la kanuni,’’ alisema Lumumba Kambere, msemaji wa M23, Kivu ya Kaskazini.
Lakini Kabila sio tu rais wa zamani kwenye karatasi. Ana mitandao ya muda mrefu ndani ya wasomi wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi nchini humo, na mwaka wa 2025 alijitokeza hadharani ndani na karibu na Goma inayoshikiliwa na waasi - kuashiria ufikiaji na ushawishi katika maeneo ya mashariki ambapo M23 na wahusika wengine wanafanya kazi.
Kwa hiyo kumhukumu kifo si adhabu tu; inaunda upya motisha za wahusika wenye nguvu mashinani.
Nani atamkamata?
Hukumu kwa kutokuwepo kwake inaweka amri ya kudumu, inayotekelezeka kwa kukamatwa kwake na madeni makubwa ya kifedha.
Kiuhalisia, hata hivyo, hatari ya moja kwa moja ya Kabila inategemea kama yuko katika eneo linalodhibitiwa na wahusika walio tayari kumkabidhi kwa DRC, na kama mataifa jirani au washirika wanamlinda inamaanisha sio jambo rahisi kutiwa pingu huko aliko.
Kwa upande mwingine uamuzi huo utapunguza vikali usafiri wa Kabila na kuongeza shinikizo kwa jimbo lolote linalomkaribisha au kumpa hifadhi.
‘‘Serikali zinazomhurumia sasa zinakabiliwa na chaguo la kidiplomasia: kumlinda mkuu wa zamani wa nchi na kuhatarisha hasira ya Kinshasa, au kujitenga na kumuweka wazi kwa kurejeshwa au kutekwa,’’ anasema Ade Daramy, mwandishi na mchambuzi wa kisiasa.
Kukimbilia mafichoni
Lakini ndani ya nchi, hukumu hii inaweza kumfaidi Kabila au kumdhuru zaidi kisiasa.
‘‘Ndani ya nchi, hukumu hiyo inaweza ama kusababisha kutengwa zaidi Kabila na washirika wake, (kupitia kutaifisha mali zao, kupigwa marufuku chama chao na kadhalika ) au-kulingana na jinsi wasimamizi wake na viongozi wa eneo hilo wanavyoitikia-kumgeuza kuwa shahidi ambaye mateso yake yanachochea kuungwa mkono na wale wanaoona mahakama kuwa na siasa. Njia ipi itatokea inategemea jinsi miundo ya chama chake na watoa mamlaka wa ndani wanavyoitikia,’’ Daramy anaambia TRT Afrika.
Kwa mujibu wa wachambuzi, uamuzi huo wa kisheria unaipa Kinshasa chombo cha kumfuatilia sio Kabila tu bali pia washirika wa karibu, wafadhili na makamanda wanaodaiwa kuunga mkono harakati za waasi. Hilo linaweza kupunguza chaguzi zake za kisiasa lakini pia linaweza kusukuma mtandao wake kuwa ya mafichoni na kuvizia.
Mashariki mwa DRC ni ngome ya makundi yenye silaha, wanamgambo wa ndani, vikosi vya usalama vya taifa na wahusika wa kigeni.
Hofu ya wananchi
Baadhi tayari wanahofia namna kesi hii ilivyofanyika inaweza kuathiri harakati zilizopo za kuleta upatanishi na kusitishwa kwa umwagaji wa damu, ikiwa ni kweli Kabila ana uungwaji mkono wa makundi hayo ya waasi.
‘‘Tunajiuliza ikiwa leo Joseph Kabila Kabange atahukumiwa, je, hukumu hii itamaliza vita mashariki mwa DRC?’’ anauliza Albert Matabaro, mmoja wa wakaazi wa Goma.
‘‘Kukamatwa kwake kunaweza kuzidisha hali ya vita. ikiwa kweli anafanya kazi na M23, watakasirika akikamatwa,’’ anasema mkaazi mwingine wa Goma, Alexis Sambuka.
Hiki sasa ni kizungumkuti kwa serikali na pia jamii ya kimataifa, kwani namna suala hili litakavyoshughulikiwa kuanzia sasa inaweza kusababisha mapokezi ya ghadhabu au ya uungwaji mkono, ndani na nje ya DRC.