| Swahili
UTURUKI
2 dk kusoma
Mawaziri wa Ulinzi wa Uturuki na Misri wakutana Ankara kuimarisha ushirikiano wa kiusalama
Uturuki na Misri zinaendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usalama, diplomasia na misaada ya kibinadamu baada ya kurejesha uhusiano wao kufuatia miaka kadhaa ya mvutano wa kisiasa.
Mawaziri wa Ulinzi wa Uturuki na Misri wakutana Ankara kuimarisha ushirikiano wa kiusalama
Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Yasar Guler, alimpokea mwenzake wa Misri, Luteni Jenerali Ashraf Salim Zahir, katika hafla rasmi jjini Ankara. / / Türkiye's Ministry of Defence

Uturuki na Misri zinaimarisha ushirikiano wa kijeshi na kikanda huku viongozi wakuu wa ulinzi wa nchi hizo wakikutana jijini Ankara, hatua inayoashiria kuimarika kwa mahusiano baada ya karibu muongo mmoja wa tofauti za kidiplomasia.

Waziri wa Ulinzi wa Taifa wa Uturuki, Yasar Guler, Jumatatu alimkaribisha Mkuu wa Majeshi ya Misri na Waziri wa Ulinzi na Uzalishaji wa Kijeshi, Luteni Jenerali Ashraf Salim Zahir, kwa hafla rasmi ya kijeshi iliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi jijini Ankara.

Baada ya nyimbo za taifa na ukaguzi wa gwaride la heshima, viongozi hao walifanya mazungumzo ya faragha yaliyojikita katika kuimarisha uhusiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili pamoja na kujadili maendeleo ya usalama katika ukanda.

Kutoka mvutano wa kidiplomasia hadi ushirikiano wa kimkakati

Mkutano huo umefanyika wakati Uturuki na Misri zikiendelea na juhudi za kurejesha kikamilifu mahusiano yao baada ya miaka ya ushirikiano finyu, huku sasa zikilenga kushirikiana zaidi katika kukabiliana na changamoto za pamoja za kikanda.

Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa nchi hizo umeimarika kwa kasi kupitia kuongezeka kwa ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Wakati wa ziara yake rasmi nchini Misri mwezi Februari, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema nchi yake inalenga kuimarisha ushirikiano na Misri katika biashara ya baharini, usafirishaji, uhuru wa usafiri wa majini na usalama wa baharini.

Erdogan pia alisisitiza kuwa mahusiano ya kiuchumi na utalii yanaendelea kukua, akibainisha kuwa ongezeko la idadi ya watalii linaonyesha mafanikio ya uhusiano huo na kueleza matumaini ya kupanua ushirikiano zaidi katika sekta ya utalii.

Ushirikiano katika kushughulikia migogoro ya kikanda

Mbali na kuimarisha uhusiano wa mataifa mawili, Uturuki na Misri zimekuwa zikiratibu juhudi katika kushughulikia migogoro mbalimbali ya kikanda, ikiwemo juhudi za kutafuta suluhu za kidiplomasia na kukabiliana na changamoto za kibinadamu.

Katika mzozo wa hivi karibuni unaohusisha Iran, Uturuki, Saudi Arabia na Pakistan zilishirikiana na Misri katika juhudi za kutafuta suluhisho ya kidiplomasia na kupunguza mvutano uliokuwa ukiongezeka.

Nchi hizo mbili pia zimeendelea kuratibu juhudi za misaada ya kibinadamu kwa Ukanda wa Gaza, zikisisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa misaada na kutumia njia za kidiplomasia kushughulikia mzozo unaoendelea.

Maafisa wa nchi hizo wanaamini kuwa kuimarika kwa ushirikiano kati ya Uturuki na Misri kutachangia utulivu wa kikanda wakati ambapo Mashariki ya Kati inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama.

 

CHANZO:TRT World