Katika miaka ya hivi karibuni Ghana imekuwa ikipigia chapuo juhudi za kuimarisha Uanamajumui huku hali ya kisiasa, kiuchumi na masuala ya tabianchi ikibadilika duniani.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limechukua hatua madhubuti kote katika bara na duniani.
Ghana ndiyo taifa pekee barani Afrika kuwapa uraia watu wenye asili ya Afrika wanaoishi nje ya bara.
Mpango huo kwa Waafrika wanaoishi nje ya nchi, unaojulikana kama "Zaidi ya kurudi Nyumbani", ulizinduliwa 2016.
Lengo ni kuungana tena na vizazi vya asili ya Kiafrika vilivyopelekwa enzi za biashara ya utumwa.
Tangu kuanza kwa mpango huo muongo mmoja uliopita, karibu hati 1,000 za kusafiria zimetolewa kwa watu wa nje "wa kihistoria", ikiwemo watu maarufu, IShowSpeed akiwa wa hivi karibuni kupata pasi hiyo.
Hatua ya kipekee
Wakati huo huo, 25 Machi 2026, Rais wa Ghana John Mahama aliwasilisha muswada wa Uanamajumui katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ikiitaja biashara ya utumwa kuwa "uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya ubinadamu katika historia ya dunia" na kutaja walipwe fidia.
Ghana iliwasilisha na Umoja wa Mataifa ukaupokea licha ya pingamizi kutoka kwa mataifa ya Magharibi, ambayo yalihusika na biashara hiyo ya utumwa kati ya karne za 16 na 18, kuharibu maisha ya mamilioni ya Waafrika.
Ghana ni mfano mzuri ambao unahitaji kupongezwa na kuigwa wa kufufua matumaini ya Afrika katika maeneo yote, Romaric Lucien Badoussi, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Parakou nchini Benin, anasema.
"Ni kweli Ghana iliungwa mkono na mataifa mengine katika mpango huu, lakini ni Ghana ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele. Na hilo lazima litambuliwe," Badoussi aliiambia TRT Afrika.
Viza bila malipo kwa Waafrika wote
"Kile kinachofanya muswada huu wa Umoja wa Mataifa kuwa muhimu wakati huu, unaelezwa kwa uwazi kuwa huu ni uhalifu mbaya uliofanywa dhidi ya ubinadamu," Badoussi aliongeza.
Nchi hiyo ya Afrika Magharibi pia imeondona malipo ya viza kwa raia wote wa Afrika, kufanya iwe rahisi kuingia nchini humo.
Mpango huo unaotarajiwa kuanza kufanya kazi 25 Mei 2026, ni sehemu ya mkakati wa Ghana kuchagiza watu kusafiri bila viza kote barani Afrika, huku Rais John Mahama, ambaye amekuwa akipigia chapuo Uanamajumui, akisema Ghana "ina jukumu la kihistoria kuruhusu Waafrika wote kutoka barani kuingia nchini mwao."
Waziri wa Mambo ya Nje Sam Okudzeto Ablakwa pia anasema, kwa sera hiyo ya viza, nchi inataka kujithibitisha kama "taifa asili la Uanamajumui."
Harakati za kutafuta uhuru
"Nimechagua Ghana kwa sababu zamani niliskia mambo mazuri kuhusu nchi hiyo. Nhci iko salama, hakuna ubaguzi. Pia, suala la msingi zaidi gharama za maisha ni nafuu," Rebecca Maria Mbourou Mombo, raia wa Gabon aliyesoma katika nchi hiyo na amekuwa akifanya kazi kama mwanasaikoljia, ameiambia TRT Afrika.
Mji wa Accra pia umekuwa mwenyeji wa mikutano mingi kuhusu Uanamajumui katika miezi ya hivi karibuni, ikiwemo kuhakikisha bara hili linakuwa na uhuru na udhibiti juu ya raslimali zake nyingi, huku Burkina Faso, Mali na Niger ikitaka kuanzisha sera kama hiyo.
Huku Ethiopia ikisifiwa kufanikiwa kukabiliana na ukoloni wa nchi za Ulaya, ikihakikisha kuwa haikutawaliwa na kuhamasisha Uanamajumui na harakati za ukombozi kote Afrika, Ghana pia ina nafasi muhimu katika historia.
Ilikuwa taifa la kwanza la Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata uhuru.
Hiyo ilikuwa 1957 chini ya Mwanamajumui Kwame Nkrumah, ambaye alikuwa rais wa nchi hiyo wa kwanza, na kuongeza umuhimu wa Uanamajumui.
Zaidi inahitajika kufanywa
Ghana inasema ndoto ya Nkrumah ya "Afrika moja, dhamira moja" ndiyo sasa inafufuliwa.
Licha ya vijana wa Kiafrika kuwa na uelewa ndani na nje ya bara, wachambuzi wanasema kuna haja ya kufanya zaidi kutimiza lengo la Uanamajumui, ikiwemo utambulishi na uritji wa kizazi cha sasa pamoja na sera thabiti za uchumi na siasa ambazo zitaimarisha maisha ya wananchi.
"Naamini uhalisia wa Uanamajumui ni umoja, msaada wa dhati, na ushirikiano miongoni mwa watu wenye asili ya Afrika pande zote mbili za Atlantiki na maeneo mengine duniani. Kwa hiyo, kwanza, serikali zisisitize hili, na mifumo yetu ya elimu iwape wanafunzi na watoto mafunzo haya ili wakuwe na wazo hili — hili ni la msingi pamoja na umoja wa watu wenye asili ya Afrika," Badoussi anapendekeza.
"Lazima turudishea Uanamajumui kwa muktadha wake wa kihistoria. Lazima tuweke wazi malengo yake na, zaidi ya yote, kuwapa mafunzo vijana na watoto kuwa Uanamajumui ni kuimarisha mshikamano wa watu wenye asili ya Afrika na kupenda watu wa bara la Afrika — hilo siyo kuhusu kuchukia au kuwakataa wengine," alisisitiza.


















