Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan atafanya ziara rasmi ya siku mbili nchini Bangladesh siku ya Ijumaa kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh Khalilur Rahman, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia.
Vyanzo hivyo vinasema kuwa ziara hiyo ya Ijumaa na Jumamosi itakuwa ya kwanza kwa Fidan nchini Bangladesh. Wakati wa ziara yake, anatarajiwa kulakiwa na Waziri Mkuu wa Bangladesh Tarique Rahman na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje Khalilur Rahman.
Fidan pia anatarajiwa kutembelea kambi ya wakimbizi mjini Cox's Bazar, ambapo kuna Waislamu milioni 1 wa Rohingya ambao walikimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Myanmar.
Anatarajiwa kukagua miradi iliyofanywa na Shirika la Uturuki la Ushirikiano na Uratibu (TIKA), Mamlaka ya Majanga na Dharura (AFAD), Hilali Nyekundu ya Uturuki, Wakfu wa Diyanet wa Uturuki na Wizara ya Afya ya Uturuki, na kutembelea Hospitali ya Kituruki inayoendesha shughuli zake kwenye kambi.
Wakati wa mikutano yake, Fidan anatarajiwa kumpongeza Rahman kwa kuchaguliwa kwake rais wa Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa.
Masuala mbalimbali yatajadiliwa
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki anatarajiwa kusisitiza ushirikiano kati ya Uturuki na Bangladesh na kueleza kuridhishwa na kasi ambayo uhusiano wa mataifa mawili inavyoendelea chini ya serikali mpya ya Bangladesh, ambayo iliingia madarakani mwezi Februari.
Fidan pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi ushirikiano katika biashara, ulinzi, nishati, elimu, utamaduni, sayansi na afya, huku akithibitisha kuhusu lengo la pamoja la kuongeza kiwango cha biashara ya mataifa hayo mawili kutoka dola bilioni 1.35 mwaka 2025 hadi dola bilioni 2.
Anatarajiwa kusisitiza kuhusu dhamira ya Uturuki kuendeleza suala la Rohingya kuwa miongoni mwa vipaumbele katika agenda ya ulimwengu na kueleza kuhusu msaada wa Uturuki tangu kuanza kwa tatizo hilo, ikiwemo msaada katika sekta ya afya, elimu, makazi, chakula na miundombinu.
Fidan anatarajiwa kusisitiza kuwa Uturuki itaendelea na juhudi za kutoa misaada.
Waziri huyo pia anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kimkakati wa Bangladesh katika uthabiti, amani na usalama Asia Kusini, akieleza kuhusu eneo lake la kimkakati na jukumu lake katika kanda.
Anatarajiwa kueleza umuhimu wa Uturuki kwa ushirikiano na Bangladesh katika maeneo mbalimbali, hasa Umoja wa Mataifa, Shirika la Ushirikiano wa Mataifa ya Kiislamu (OIC) na Shirika la D-8 la Ushirikiano wa Kiuchumi.
Pande hizo mbili pia zinatarajiwa kushauriana kuhusu masuala ya kikanda na dunia, ikiwemo yanayojiri sasa Mashariki ya Kati, Iran na Asia Kusini.
Serikali mpya ya Bangladesh iliingia madarakani kufuatia uchaguzi wa Februari 12. Uturuki iliwakilishwa katika hafla ya uapisho Februari 17 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Berris Ekinci, ambaye alilakiwa na Waziri Mkuu Rahman na pia kukutana na kiongozi wa chama cha Jamaat-e-Islami Shafiqur Rahman.
Uhusiano wa mataifa mawili
Khalilur Rahman, ambaye ni waziri wa mambo ya nje wa serikali mpya iliyoundwa Februari na kuteuliwa na Bangladesh kwa urais wa Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa, alifanya ziara yake ya kwanza ya nje ya nchi katika taifa la Uturuki Machi 14 na baadaye kuhudhuria Jukwaa la 5 la Kidiplomasia la Antalya Aprili 17-19.
Msaada wa Uturuki kwa Waislamu wa Rohingya umepita zaidi ya dola milioni 80.
Msaada wa Uturuki utaendelea katika kambi za wakimbizi ambazo zina Warohingya zaidi ya milioni 1 nchini Bangladesh kupitia miradi ya afya, makazi, elimu na miundombinu ikiongozwa na TIKA, AFAD, Hilali Nyekundu ya Uturuki na Wakfu wa Uturuki wa wa Diyanet.
Hospitali ya Uturuki iliyoanzishwa jijini Cox's Bazar mwaka 2018 inaendelea kutoa huduma za afya kwa wagonjwa karibu 1,000 kila siku, ikiwemo raia wa Bangladesh. Hospitali hiyo inaajiri wafanyakazi 85, ikiwemo raia 30 wa Uturuki na 55 wa Bangladesh.
Zaidi ya hayo miradi inayofanywa na taasisi za Uturuki kama vile TIKA, Wakfu wa Uturuki wa Diyanet na Hilali Nyekundu ya Uturuki, Shirika lisilokuwa la kiserikali la Kituruki pia yanatekeleza miradi ya misaada kwa wakimbizi wa Rohingya na raia wa Bangladesh, ikiwemo kutoa misaada ya chakula, futari wakati wa Ramadhan na kuchinja wanyama wakati wa sikukuu ya Eid al Adha.





















