| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Misri ‘yaigomea’ Ethiopia kujenga mabwawa mapya ndani ya mto Nile
Uamuzi huo, unatokana na mgogoro unaotakana na Ethiopia, kudaiwa kukiuka makubaliano yaliyowekwa ndani ya mkataba wa GERD, kwa mujibu wa Waziri wa Umwagiliaji wa Misri, Hani Sewilam.
Misri ‘yaigomea’ Ethiopia kujenga mabwawa mapya ndani ya mto Nile
Serikali ya Misri imesisitiza kuwa haitoiruhusu Ethiopia kujenga mabwawa mapya ndani ya mto Nile.

Serikali ya Misri imeitaka Ethiopia kuheshimu na kuzingatia makubaliano ya GERD, baada ya Ethiopia kudaiwa kutaka kujenga mabwawa matatu zaidi kwenye mto huo.

Serikali ya Misri imesisitiza kuwa haitoiruhusu Ethiopia kujenga mabwawa mapya ndani ya mto Nile.

Uamuzi huo, unafuatia na madai ya Ethiopia ya kukiuka makubaliano yaliyowekwa ndani ya mkataba wa GERD, kwa mujibu wa Waziri wa Umwagiliaji wa Misri, Hani Sewilam.

Kauli ya Sewilam inakuja wiki mbili baada ya kuibuka kwa taarifa zinazodai kuwa Ethiopia inapanga kujenga mabwawa mapya matatu ndani mto huo mrefu zaidi duniani.

"Ni wazi kuwa Ethiopia inalenga kujenga mabwawa hayo, na sisi hatutokubali,” alisema waziri huyo.

Sewilam, amesisitiza kuwa, nchi yake imekuwa ikiikumbusha Ethiopia kuheshimu mkataba wa GERD kwa ajili ya mustakabali wa mradi huo.

Waziri huyo, amedai kuwa, uamuzi huo unaweza kuiathiri Sudan, na kuifanya nchi huyo kushindwa kuendesha na kusimamia mabwawa yake.

"Si vyema kuilaumu Sudan kwa lolote lile, kosa ni la Ethiopia kwa kushindwa kuheshimu mkataba na makubaliano yaliyowekwa,” alisema.

Sewilam ameongeza kuwa Misri, itaendelea kuheshimu na kuzingatia mkataba na makubaliano ya GERD, kama yalivyowekwa.

Hata hivyo, hapakuwa na taarifa yoyote kutoka kwa serikali ya Ethiopia kuhusiana na madai ya Misri.

Kwa pamoja, Misri na Sudan zimekuwa katika mvutano mkubwa na Ethiopia kuhusu ujazaji wa mabwawa ya mradi huo wa GERD, ambao ulianza kujengwa mwaka 2011.

Mvutano huo, ulisababisha kusitishwa kwa mazungumzo kwa kipindi cha miaka mitatu, kabla ya kuanza tena mwaka 2024.

Mto Nile, ambao unakadiriwa kuwa na urefu wa kilomita 6,650, unanufaisha jumla ya nchi 11 za Afrika, ambazo ni Burundi, Rwanda, DRC, Kenya na Uganda.

Nyingine ni Tanzania, Ethiopia, Eritrea, Sudan Kusini, Sudan na Misri.