Waziri wa Madini nchini Tanzania, Anthony Mavunde amesema kuongezeka kwa uwekezaji kwenye sekta ya madini kumechangia ongezeko la pato la taifa kwa asilimia 11.9.
Akizungumza wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya mapato ya matumizi ya wizara yake kwa 2026/2027, Aprili 27, 2026, Bungeni jijini Dodoma, Mavunde amesema mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka.
"Mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka,” alisema Mavunde.
Kulingana na Mavunde, mchango huo uliongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.
Aidha, hadi kufikia kipindi cha robo tatu ya mwaka 2025, wastani wa mchango wa sekta ya madini, ulikuwa umefikia asilimia 11.9.
“Mwenendo huu umechangiwa na kuongezeka kwa uwekezaji katika Sekta ya Madini," alieleza.
Wakati huo huo, Mavunde ameongeza kwa kusema kuwa Tanzania inalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza ushindani wa nchi katika sekta ya madini duniani na kuvutia mitaji zaidi kupitia mageuzi ya kisera.
Hali kadhalika, ameliomba Bunge la nchi hiyo limuidhinishie bajeti ya Shilingi 224.98 bilioni kwa ajili ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.













