Erdogan atunukiwa Tuzo ya 'WHO Europe' kwa juhudi za kibanadamu za Uturuki nchini Palestina
Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Afya Duniani (WHO) barani Ulaya, Hans Kluge, amemkabidhi Rais Recep Tayyip Erdogan tuzo hiyo katika Mkutano wa 11 wa Kimataifa wa Tiba wa Uturuki uliofanyika Ankara.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amepokea Tuzo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Ulaya kwa ajili ya juhudi za kibinadamu za Uturuki kwa watu wa Palestina na mchango wake katika kuwezesha uokoaji wa wagonjwa kutoka Ukanda wa Gaza.
Tuzo hiyo iliwasilishwa na Hans Kluge, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Ulaya, wakati wa Mkutano wa 11 wa Kimataifa wa Tiba wa Uturuki jijini Ankara siku ya Jumatano.
Katika hotuba yake kwenye hafla hiyo, Erdogan alikosoa ukimya wa jumuiya ya kimataifa kuhusu uharibifu wa hospitali na mauaji ya wagonjwa, wahudumu wa afya na watoto wachanga huko Gaza katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
“Bila shaka haitakuwa rahisi kwa dunia kuondokana na hali halisi ambapo kwa miaka miwili kamili imekuwa mtazamaji huku hospitali zikilipuliwa Gaza na wagonjwa, wahudumu wa afya, watoto, na hata watoto wachanga waliokuwa kwenye kisanduku cha joto (inubator) wakiuawa,” alisema.
Erdogan aliongeza kuwa dunia ingekuwa “pepo” siku ambayo binadamu wote watashirikiana katika furaha ya kuokoa uhai na kusherehekea kuzaliwa kwa kila mtoto kama furaha ya pamoja.
“Hii ndiyo hasa tunayoifanyia kazi,” alisema.
Erdogan alisema Uturuki imefanya mageuzi makubwa katika mfumo wake wa afya kwa kipindi cha miaka 23 iliyopita, na kuugeuza kuwa mtandao mpana, wenye ubora wa juu na unaoafikika kwa watu wote.
Alibainisha kuwa nchi hiyo sasa inatoa huduma za kiwango cha juu kwa watu milioni 86 kwa msaada wa zaidi ya watumishi wa afya milioni 1.47.
Juhudi bunifu na za kweli
Alisema pia kuwa nguvu kazi ya sekta ya afya imeongezeka kwa asilimia 288 tangu mwaka 2002, na kwamba karibu wafanyakazi 100,000 wapya, wakiwemo zaidi ya madaktari 57,000 wameajiriwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita.
Aliongeza kuwa asilimia 80 ya hospitali za umma zimekarabatiwa au kujengwa upya, huku hospitali mpya 794 zikiongeza uwezo wa vitanda vya umma hadi kufikia 173,000. Idadi ya vitanda vyenye ubora wa juu imeongezeka kutoka 7,000 mwaka 2002 hadi 122,000 leo, na uwezo kwa jumla kupanuka kutoka 164,000 hadi 271,000.
Erdogan alisisitiza pia kuendelea kwa ujenzi upya katika mikoa iliyoathirika na tetemeko la ardhi, ambako vituo vya afya 109 vyenye zaidi ya vitanda 5,100 vimekamilika, na kuongeza uwezo wake kwa jumla kutoka 23,733 hadi 27,503 katika mikoa 11.
Alisisitiza umuhimu wa Uturuki kupiga hatua katika utafiti wa kisayansi, uzalishaji wa dawa, na utengenezaji wa vifaa vya tiba.
“Licha ya vikwazo vya ndani na nje, naamini tutafanikiwa katika teknolojia za afya kama tulivyofanikiwa katika tasnia ya ulinzi,” alisema, akiongeza kuwa Uturuki itaendelea kuunga mkono juhudi zote bunifu na zenye uhalisia zinazoendeleza malengo yake ya huduma za afya.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki, Burhanettin Duran, pia alitoa maoni kuhusu tuzo hiyo kupitia jukwaa la kijamii la NSosyal, akisema utambuzi huo “ni ushahidi wa diplomasia ya kibinadamu ya Uturuki inayoongozwa na maono ya Rais wetu.”
Aliongeza: “Licha ya hali mbaya huko Gaza, kuendelea kwa misaada ya kibinadamu, uokoaji wa wagonjwa kwa usalama, na kutetea wanaoonewa kumewezekana kupitia ufuatiliaji binafsi, nia na uongozi wa rais wetu. Umakini wake wa muda mrefu kuhusu suala la Palestina unaendelea kuleta athari kubwa katika eneo na kwenye majukwaa ya kimataifa.”