Vazi la kitamaduni la fugu kuvaliwa kila Jumatano nchini Ghana
Madhumuni ni kuenzi upekee wa vazi hilo la nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Kuanzia sasa, nchini Ghana, kila Jumatano raia wa nchi hiyo watakuwa wanavaa vazi lao la kitamaduni liitwalo fugu.
Hii ni baada ya serikali ya Ghana kutangaza kuwa, kila Jumatano itakuwa ni ya fugu kuanzia Februari 10.
Madhumuni ni kuenzi upekee wa vazi hilo la nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Haya yanajiri baada ya Rais wa Ghana John Dramani Mahama mapema mwezi Februari kuitembelea Zambia akiwa amevaa vazi la fugu, jambo lililodhihakiwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Zambia.
Katika maeneo ya kaskazini mwa Ghana vazi hilo linajulikana kama Batakari kati ya kabila la Akan na Fugu kati ya Dagomba, Mamprusi, na vikundi vyengine vya kaskazini.
Kwa kawaida, vazi hilo linasimama kama alama ya kujivunia na utambulisho thabiti kwa umoja wa taifa.
Vazi hili la jadi, linalofumwa kwa mkono kwa kutumia pamba nene na kuunganishwa kwa uangalifu katika umbo linalofanana na kanzu.
Kwa watu wa Ghana ni zaidi ya vazi; ni kauli ya utu inayowakilisha ustadi wa ufundi wa kaskazini na urithi wa taifa.
Ghana inahusisha asili yake kuanzia jamii za awali kaskazini, ambapo ufumaji uliibuka kama aina ya sanaa na kitamaduni.
Fugu, hata hivyo, ilipata umaarufu zaidi Machi 1957 wakati Rais wa kwanza wa Ghana Kwame Nkrumah na baadhi ya viongozi wengine walipovaa wakati wa sherehe ya kuapishwa kwa uhuru wa nchi hiyo.
Hali ya hewa kavu ya eneo hilo na uzalishaji mkubwa wa pamba ulihimiza ukuzaji wa vitambaa vilivyosokotwa kwa mkono na kufumwa vyema ambavyo vilitoa kinga dhidi ya jua na upepo.
Hapo awali, fugu ilivaliwa na wawindaji na wapiganaji ambao walithamini nguvu zake na ishara ya kiroho.
Kwa sasa, fugu mara nyingi huhusishwa na wanaume, ambao wakati mwingine huvaa suruali inayofanana na kofia, lakini wanawake pia huvaa aina tofauti na muundo huu.
Leo, huvaliwa kwenye sherehe, na wafanyakazi wa serikali na inazidi kuwa mtindo wa kisasa.
Na sasa Rais wa Ghana ameazimia kunadi uzuri na upekee wa fugu kwa ulimwengu wote, kwa yeye mwenyewe kuwa mstari wa mbele katika kuiva.