Ni siku moja tangu Serikali ya Tanzania iwasilishe Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 yenye thamani ya shilingi trilioni 62.33, lakini mjadala kuhusu uwezo wake wa kujibu changamoto za maisha ya wananchi unaendelea kushika kasi ndani na nje ya Bunge.
Bajeti hiyo, ambayo ni ya kwanza kutekelezwa chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, imejengwa katika mkakati wa kuharakisha ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji katika miundombinu, mageuzi ya kidijitali na kuimarisha uzalishaji wa ndani.
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar, alisema Serikali imeandaa mpango huo kwa lengo la kuharakisha ukuaji wa uchumi, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Serikali inaeleza kuwa hatua hizo zinalenga kuongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania na kuimarisha uwezo wa nchi kujitegemea katika kugharamia maendeleo yake.
Pamoja na matarajio hayo, baadhi ya wananchi waliozungumza na TRT Afrika wanasema bado hawajaona namna bajeti hiyo itakavyotoa majibu ya moja kwa moja kwa changamoto za kila siku zinazowakabili.
Warda Waziri, mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dodoma, amesema bado hajaona hatua za kutosha za kupunguza mzigo wa gharama za maisha.
"Haijazingatia kwa kiwango kikubwa uhalisia wa Watanzania wa kawaida, hasa kwenye suala la gharama za maisha na bei ya mafuta," amesema.
Hata hivyo, Hamiss Rajabu anaamini bajeti hiyo imeonyesha mwelekeo wa kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa vijana kupitia maboresho mbalimbali ya sera na kodi.
"Kuna dalili kwamba vijana wengi wanaweza kupata nafasi zaidi za kuanzisha na kukuza biashara zao," amesema.
Maoni hayo yanafanana na maoni ya baadhi ya wabunge, ambapo baaadhi tuliozungumza nao wametoa tathmini zao kuhusu mapendekezo hayo.
Miongoni mwao ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia ACT Wazalendo, Kiza Mayeye. Amesema bado hajaona bajeti hiyo ikitoa majibu ya kutosha kwa changamoto zinazowakabili wananchi wengi.
"Bado sijaona kama bajeti inaenda kujibu matatizo ya Watanzania," amesema, akitaja ugumu wa maisha na changamoto zinazowakabili vijana pamoja na sekta ya usafiri wa bodaboda.
Kwa upande wake, Mbunge wa Katavi kupitia CCM, Thomas Kampala Maganga, amesema bajeti hiyo inaonyesha dhamira ya kuimarisha uchumi unaotegemea zaidi mapato ya ndani.
"Mwelekeo mkuu wa bajeti hii ni kuendelea kujenga uwezo wa nchi kujitegemea kiuchumi," amesema, huku akieleza kuwa mjadala wa bunge utatoa nafasi ya kufafanua zaidi maeneo mbalimbali yaliyowasilishwa.
Wakati Serikali ikisisitiza kuwa bajeti hiyo itachochea uwekezaji, uzalishaji na ajira, macho ya wananchi sasa yanaelekezwa katika utekelezaji wake na matokeo yatakayojitokeza katika maisha yao ya kila siku.
Kwa wengi, mtihani halisi wa Bajeti ya 2026/27 hautakuwa kwenye takwimu za trilioni zilizotangazwa bungeni, bali katika uwezo wake wa kupunguza gharama za maisha, kuongeza ajira na kuboresha ustawi wa mwananchi wa kawaida.


















