Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kimeitisha kikao cha dharura cha ngazi ya juu ya uratibu, kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mkutano huo utakaofanyika Mei 15, 2026, utashirikisha mamlaka za afya za DRC, Uganda, Sudan Kusini pamoja na washirika muhimu ikiwemo, Shirika la Afya Duniani (WHO), kijadili namna za kukabiliana na mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola uliothibitishwa katika jimbo la Ituri, DRC.
Takwimu zinaonesha kuwa kuna takriban maambukizi 246 yaliyoripotiwa na vifo 65, hususani katika maeneo ya Mongwalu na Rwampara.
Vifo vinne vilivyoripotiwa, vilitokana na maambukizi yaliyothibitishwa na maabara.
Ugonjwa wa virusi vya Ebola ni hatari na mara nyingi unasababisha vifo.
Huenea kwa kugusana moja kwa moja na maji maji ya mwili ya watu walioambukizwa, vifaa vyenye maambukizi, au watu waliokufa kutokana na maradhi hayo.
Kufuatia mashauriano na Wizara ya Afya ya DRC na Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Umma, matokeo ya awali ya maabara kutoka Institut National de Recherche Biomédicale (INRB) yaligundua virusi vya Ebola katika sampuli 13 kati ya 20 zilizopimwa.
Matokeo ya maabara yanaonesha uwepo kwa virusi vya Ebola ambavyo si vya aina ya Zaire, huku uchunguzi wa kisayansi zaidi ukiendelea ili kubainisha zaidi mlipuko huu mpya.
Matokeo yanatarajiwa kuwekwa wazi ndani ya saa 24 zijazo kwa msaada kutoka Africa CDC.
Mkutano kati ya Afrika CDC, nchi jirani za DRC na wadau wengine muhimu wa afya utazingatia vipaumbele vya majibu ya haraka, uratibu wa mipaka, ufuatiliaji, msaada wa maabara, kuzuia na kudhibiti maambukizi, mawasiliano ya hatari, mazishi salama na yenye heshima, na ukusanyaji wa rasilimali.
"Afrika CDC inasimama na serikali na watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanapokabiliana na mlipuko huu," Dkt. Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Afrika CDC alisema katika taarifa iliyotolewa na Africa CDC.
"Kwa kuzingatia harakati kubwa ya idadi ya watu kati ya maeneo yaliyoathirika na nchi jirani, uratibu wa haraka wa kikanda ni muhimu. Tunashirikiana na DRC, Uganda, Sudan Kusini na washirika ili kuimarisha ufuatiliaji, maandalizi na mwitikio, na kusaidia kudhibiti mlipuko haraka iwezekanavyo."
Afrika CDC imeonesha wasiwasi wake kuhusu hatari ya kuenea zaidi ndani ya nchi hiyo, kutokana na mazingira ya mijini ya Bunia na Rwampara ambako kuna pilikapilika kubwa za watu, ikiwemo uhamaji unaohusiana na uchimbaji madini huko Mongwalu, ukosefu wa usalama katika maeneo yaliyoathiriwa, mapengo katika orodha ya mawasiliano, changamoto za kuzuia na kudhibiti maambukizi, na ukaribu wa maeneo yaliyoathiriwa na Uganda na Sudan Kusini.
Huu ni mlipuko wa 17 wa Ebola kutokea nchini DRC tangu 1976.
















