Rais wa Congo kuwania tena urais baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 40

Sheria ya nchi hiyo inamruhusu kuwania muhula mpya kufuatia mageuzi ya kikatiba mwaka 2015.

By
Rais Nguesso aliingia madarakni mwaka wa 1979 hadi 1992 na baadaye tena mwaka wa 1997. / / Reuters

Rais wa Jamhuri ya Congo (Brazzaville), Denis Sassou Nguesso, alitangaza siku ya Alhamisi kwamba atashiriki katika uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika mwezi Machi 2026, akiwa na lengo la kusalia madarakani kwa zaidi ya miongo minne huku akiwa na umri wa miaka 82.

"Nitashiriki kama mgombea katika uchaguzi wa urais," alisema kiongozi wa nchi hiyo katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rais huyo alitangaza azma yake mbele ya umati wa maelfu ya watu katika wilaya ya kusini ya Ignie.

Kisheria, Nguesso hana kizuizi cha kushiriki katika uchaguzi huo. Marekebisho ya katiba yaliyopitishwa mwaka 2015 yameondoa kizuizi cha umri cha awali cha umri wa miaka 70 kwa wagombea urais na kuanzisha mfumo wa mihula mitatu ya miaka mitano.

Nguesso ameiongoza Jamhuri ya Congo, inayojulikana pia kama Congo-Brazzaville, katika mfumo wa chama kimoja tangu 1979 hadi 1992, kabla ya kushindwa na Pascal Lissouba katika uchaguzi wa kidemokrasia wa kwanza. Alirudi tena madarakani mwaka wa 1997 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, na amekua akiongoza nchi hiyo hadi sasa.

Chama tawala Congolese Labour Party (PCT) kilitangaza Disemba mwaka jana kwamba rais atawania muhula mpya.

Nguesso alishinda tena katika uchaguzi wa Machi 2021 kwa zaidi ya asilimia 88 ya kura.