Rais wa Kenya, William Ruto, siku ya Jumatano alitetea rekodi ya utawala wake katika nyanja za uchumi, maendeleo, na utoaji wa huduma kwa umma, alipohutubia kikao cha pamoja cha Bunge katika hotuba yake ya nne kuhusu Hali ya Taifa.
Katika hotuba yake, Ruto alisisitiza masuala yanayohusu uboreshaji wa uchumi, maendeleo ya ugatuzi, na usawa, huku akielezea maendeleo na vipaumbele vya serikali yake kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 2027.
"Tumefanya kazi ya kupunguza gharama za bidhaa na huduma muhimu, huku tukiongeza tija, kutengeneza ajira, na kupanua fursa za biashara," alisema.
Rais alielezea juhudi za mahsusi za serikali yake katika kusaidia sekta zote za uchumi, ikiwemo biashara ndogo na za kati.
"Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kutoka Chini kwenda Juu (Bottom-Up) pia imeweka kipaumbele katika kusaidia biashara ndogondogo, kuunda ajira, na kuendeleza miundombinu ili kujenga uchumi wenye tija zaidi," Rais aliwaambia wabunge.
Ruto pia alizungumzia suala la ushirikishwaji wa Wakenya wote, akisisitiza kuwa sauti ya kila Mkenya inapaswa kusikilizwa ili kufikia ustawi wa pamoja.
"Matamanio yangu makuu—ndoto ya kujenga Kenya ambapo kila raia ana thamani, kila jamii inahisi kuwa ni sehemu ya taifa, na hakuna Mkenya anayeachwa nyuma—yanaanza kutimia. Kiini cha dhamira hii ni 'usawa'. Kenya hiyo, ambapo fursa haiamuliwi na wewe ni nani au unatoka wapi, imefika. Hii haikutokea kwa bahati mbaya, bali kupitia juhudi za makusudi," Rais aliongeza.
Rais Ruto alionyesha fahari yake kuhusu kasi ya kufufuka kwa uchumi wa nchi chini ya uongozi wa serikali yake, akisema, "Kenya inafanya urejesho mkubwa na imara."
Hotuba hiyo inakuja wakati kukiwa na wasiwasi miongoni mwa wananchi kuhusu gharama ya maisha, ukosefu wa ajira, kodi, na ongezeko la deni la taifa; huku upinzani ukitarajiwa kuchunguza kwa kina utendaji wa serikali.
Aidha, hotuba yake inatolewa wakati wanasiasa kutoka pande mbalimbali wakiwa tayari wameanza kampeni zisizo rasmi za uchaguzi kote nchini, huku taifa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.





















