Uingereza siku ya Alhamisi iliweka vikwazo dhidi ya kile ilichosema ni mitandao haramu ya biashara ya dhahabu na fedha inayochochea vita vya Sudan, kwa kuwawekea vikwazo watu binafsi na taasisi 11.
Vita hivyo vilianza mwaka 2023 kati ya Jeshi la Sudan na kikosi cha RSF, na vimesababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makazi yao.
Vikwazo vya Uingerea vinamlenga mfadhili mmoja wa RSF ambaye anashukiwa kusaidia kufadhili shughuli za kundi hilo kupitia mtandao wa kampuni za biashara ya ardhi na nyumba, dhahabu na kampuni za uwekezaji zilizoko Dubai.
Walioorodheshwa pia katika vikwazo hivyo ni maafisa wanaohusika na ununuzi wa vifaa kwa niaba ya RSF pamoja na kampuni mbili zilizosajiliwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Ukatili wa mauaji ya halaiki
Vikwazo hivyo vinajumuisha kampuni moja yenye makao yake Hong Kong ambayo Uingereza imesema inahusishwa na ufadhili wa vita hivyo.
Jumatatu, Umoja wa Ulaya pia uliweka vikwazo dhidi ya sekta ya biashara ya dhahabu ya Sudan kutokana na vita vinavyoendelea nchini humo.
Kwa mujibu wa Uingereza, mauzo rasmi ya dhahabu ya Sudan yalikuwa na thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 1.5 katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2025. Hata hivyo, ilikadiria kuwa dhahabu yenye thamani ya mabilioni ya Dola husafirishwa kwa magendo kwenda nje ya nchi kila mwaka kupitia njia haramu.
Uingereza pia ilionya kuwa mji wa Al Obeid, ulioko katikati mwa Sudan na wenye umuhimu wa kimkakati, uko katika hatari ya kushuhudia mauaji ya kikatili kwa kiwango kikubwa, na ikatoa wito kwa Umoja wa Mataifa kupanua marufuku ya usambazaji wa silaha ili lijumuishe eneo hilo.

















