Mfanyabiashara wa Tanzania Rostam Aziz amenunua shirika kubwa zaidi la habari Afrika Mashariki, Nation Media Group (NMG), kutoka kwa familia ya Aga Khan, chombo hicho kilisema siku ya Jumanne.
Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Aga Khan (AKFED), kupitia kampuni ya NPRT Holdings Africa Limited (NPRT), ulikuwa unamilikia asilimia zaidi ya 54% ya hisa zote za NMG, kufanya AKFED kuwa mwenye hisa nyingi zaidi.
Mfanyabiashara Aziz, 61, kupitia kampuni yake ya Taarifa Limited, amenunua hisa zote za AKFED huko NMG, gazeti la Nation la Kenya limeripoti.
Kimsingi yeye ndiye mwenye hisa nyingi zaidi. Rostam Aziz, ambaye ni mfanyabiashara katika sekta ya mawasiliano, vyombo vya habari, kilimo,masuala ya bandari, nishati, madini, na ujenzi.
Matatizo ya kifedha
Tangu kuanzishwa kwake nchini Kenya 1959, kampuni ya Nation Media Group imehusishwa na familia ya Aga Khan. Ilipoanzishwa, Nation ilikuwa inachapisha gazeti la Taifa Leo kwa lugha ya Kiswahili, ambayo inazungumzwa na watu wengi nchini Kenya na mataifa jirani, ikiwemo Tanzania.
Shirika hilo la habari linamiliki vituo vya televisheni NTV Kenya na NTV Uganda; gazeti la Nation, ambalo linaongoza kwa mauzo nchini Kenya; gazeti la kila wiki la The East African regional; Business Daily nchini Kenya; Daily Monitor nchini Uganda; The Citizen nchini Tanzania, vituo vya redio, mitandao ya kidijitali, na masuala mengine katika tasnia ya habari.
Kwa miongo kadhaa, NMG, ambayo inategemea mapato yake kutoka kwa matangazo, ilikuwa inapata faida kubwa, lakini kutokana na kuibuka kwa mifumo ya kidijitali, kampuni hiyo imekuwa na matatizo ya kifedha katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa mfano, mwaka 2023, ilipata hasara ya shilingi za Kenya milioni 203 ( dola milioni $1.6), na mwak uliofuata, hasara ikawa kubwa zaidi ya shilingi milioni 254 ( dola milioni $2).
Aziz anatarajia kupata faida
Mmiliko mpya wa kampuni hiyo, Aziz, anatumai kuwa atabadilisha muelekeo na kupata faida kutokana "na uwekezaji zaidi na mabadiliko ya kidijitali," taarifa ya pamoja kutoka kwa AKFED na Taarifa Limited ilisema Jumanne.
Kampuni ya Taarifa Limited imeahidi kulinda "utamaduni wa muda mrefu wa uandishi wa habari kwa maslahi ya umma." wa NMG
Uuzaji wa NMG unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne, iwapo utaidhinishwa na taratibu za uratibu, gazeti la Nation liliripoti siku ya Jumanne.
Mtanzania wa kwanza kuwa bilionea wa dola za Marekani
Kulingana na African Financials, NMG ilikuwa na wafanyakazi zaidi ya 1,100 kufikia mwaka 2024.
Mmiliki mpya wa kampuni, Rostam Aziz, alikwua Mtanzania wa kwanza kuwa bilionea wa dola mwaka 2013, kulingana na viwango vya Forbes. Kufikia 2015, thamani yake ilikuwa imeshuka hadi dola milioni $900. Taarifa za thamani yake ya sasa hazifahamiki.




















