Tamasha la uvuvi la Argungu latia fora Nigeria
Tamasha la Uvuvi la Argungu lafana nchini Nigeria./Picha:Wengine
Tamasha la uvuvi la Argungu latia fora Nigeria
Tamasha hilo ni moja ya vivutio vikubwa vya kitamaduni, kulingana na UNESCO.
tokea masaa 11

Samaki mwenye uzito wa kilo 59 amegonga vichwa vya habari nchini Nigeria, baada ya kuvuliwa katika tamasha la kitamaduni na uvuvi la Argungu, lililofanyika nchini humo.

Tamasha hilo lililofanyika katika jimbo la Kebbi lilikamilika Jumamosi ya Februari 14, baada ya kusitishwa kwa miaka sita.

Zaidi ya wavuvi 50,000 kutoka Nigeria, Niger, Cameroon, Chad na Togo walishiriki tamasha hilo lililovutia mamia ya watazamaji.

Katika tamasha hilo, Abubakar Usman, mvuvi wa samaki kutoka jimbo la Kebbi aliibuka mshindi, kwa kufanikiwa kumpata samaki mwenye uzito wa kilo 59.

Usman alizawadiwa kitita cha Dola za Kimarekani 739, kufuatia ushindi wake.

Kukuza utalii

Kwa upande wake, rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa tamasha hilo, alifurahishwa na tukio hilo, akiliita la kihistoria.

Hali kadhalika, aligusia umuhimu wa kukuza utamaduni, utalii, kilimo na biashara.

Tamasha hilo lilinogeshwa na watumbuizaji wa siku hiyo, na kulifanya tukio hulo kuwa kivutio kingine cha utalii.

Tamasha hilo lilifanyika mara ya mwisho mwaka 2020, kabla ya kusitishwa kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19.

Liliandaliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1934 na kiongozi wa jadi wa wakati huo, Muhammad Sama, kuadhimisha miaka miwili ya uhasama kati ya jamii yake na Sultani wa Kotoko, Hassan Dan-Mu'azu.

Katika miongo kadhaa iliyopita, tamasha hilo limevutia wageni mbalimbali ulimwenguni na kugeuka kuwa sehemu ya somo kwenye mtaala wa elimu nchini Nigeria.

Mwaka 2009, tamasha hilo liliingia kwenye orodha ya shirika la UNESCO kama moja ya tamaduni na urithi usioonekana, wenye kupaswa kulindwa kwa nguvu zote.

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili