Utajiri wa Afrika: Guinea kufaidi kutoka kwa madini ya chuma

Guinea imezindua mgodi wa Simandou, huku usafirishaji wa kwanza wa madini ya chuma ukitarajiwa katika kipindi cha wiki moja.

By Coletta Wanjohi
Ukiwa na thamani ya zaidi ya dola bilioni 23, mradi wa Simandou ndio ubia mkubwa zaidi wa madini kuwahi kufanyika. / Reuters

Barani Afrika, taifa la Afrika Kusini linaongoza kwa uzalishaji wa madini ya chuma. Uzalishaji wake ulikuwa tani milioni 66 za madini ya chuma mwaka 2024. 

Madini ya chuma ni miamba na madini ambayo chuma kinaweza kuzalishwa kwa ajili ya biashara.

Madini haya yanaweza kuingizwa moja kwa moja kwenye tanuri la kutengeneza chuma.

Madini ya chuma ni malighafi inayotumika kutengeneza chuma chenyewe. Asilimia 98 ya madini ya chuma yanayochimbwa hutumika kutengeneza vyuma halisi.

Mgodi wa Kumba nchini Afrika Kusini ni mzalishaji mkubwa zaidi wa madini ya chuma barani Afrika. Kampuni hiyo ina maeneo matatu ya uzalishaji wa madini ya chuma nchini huku kampuni ya Anglo American ikimiliki asilimia 69.7 za hisa ya kampuni hiyo.

Upatikanaji wa madini haya ya chuma umepungua nchini Afrika Kusini kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, kutoka tani milioni 73.1 miaka mitatu iliyopita.

Sekta ya madini ya Afrika Kusini inakabiliana na changamoto za usafirishaji hasa kutokana na ukarabati wa reli unaoendelea.

Wazalishaji wengine wakuu barani Afrika ni pamoja na Mauritania na Algeria; wakati Zimbabwe na Morocco zikizalisha madini kwa matumizi ya ndani pekee. 

Ndiyo hifadhi kubwa zaidi duniani ambayo haijatumiwa na madini hayo yamewekwa katika kiwango cha 65% cha chuma isiyo na kaboni.

Hatua za kuendeleza mradi huo zilianza mwishoni mwa miaka ya 1990 wakati Rio Tinto, kampuni ya uchimbaji madini ya Anglo-Australia, ilipogunduwa kwa mara ya kwanza kiwango kikubwa kinachoweza kutumika kwa biashara katika milima ya Simandou. 

Tangu wakati huo, hatua zimekwamishwa kutokana na hali mbaya ya usalama na kubadilika kwa mamlaka kila mara.

Ukiwa na thamani ya zaidi ya dola bilioni 23, mradi wa Simandou ndio ubia mkubwa zaidi wa madini kuwahi kufanyika.

Unajumuisha ujenzi wa reli ya kilomita 552 inayounganisha migodi miwili mipya katika Milima ya Simandou na bandari mpya ya kina kirefu kwenye pwani ya Guinea.

Uzalishaji unatarajiwa kuongeza hadi tani milioni 120 za madini ya chuma ya kiwango cha juu kila mwaka ifikapo 2030, kiwango ambacho kitasawazisha usambazaji kimataifa kwa kiasi kikubwa.

Robo tatu ya mapato yake yataelekea China ambapo kwa sasa inamiliki asilimia 75 ya mradi wa uchimbaji madini. Serikali ya Guinea tapata 15% ya jumla ya mapato kutoka kwa kila moja ya migodi miwili  ya uchimbaji vya madini.

Ingawa kwa sasa Guinea si miongoni mwa wazalishaji wakuu wa madini ya chuma duniani, inatarajiwa kupanda hadi nafasi ya tatu punde tu migodi ya Simandou itakapofikia uwezo wake kamili nchini humo ambapo uchimbaji madini kwa sasa unachangia karibu 2.2% ya mapato ya Taifa.

Makadirio ya serikali ya Guinea yanaonyesha mradi huu wa madini ya chuma pekee unaweza kuongezea serikali mapato hadi kufikia dola bilioni 1 kila mwaka iwapo itazalisha kikamilifu kwa ajili ya biashara duniani.