Mamlaka ya Kudhibiti Mawasiliano nchini Uingereza (Ofcom) imeanzisha uchunguzi wa kubaini iwapo jukwaa la TikTok linazingatia sheria za usalama mtandaoni, ikilenga hasa hatua zake za kuthibitisha umri wa watumiaji na usalama wa watoto.
Katika taarifa yake iliyotolewa Alhamisi, Ofcom ilisema: "Uchunguzi huu utalenga kubaini iwapo kuna sababu za msingi za kuamini kwamba TikTok imeshindwa, au inaendelea kushindwa, kutimiza wajibu wake wa kisheria."
Ofcom iliongeza kuwa uchunguzi huo utazingatia kwa karibu mfumo wa TikTok wa kuthibitisha umri wa watumiaji.
Kwa upande wake, TikTok imesema ina "imani" kwamba inatimiza wajibu uliowekwa chini ya Sheria ya Usalama Mtandaoni ya Uingereza (Online Safety Act), iliyoanza kutumika mwaka jana kwa lengo la kuimarisha usalama kwa watoto.
Katika taarifa yake, msemaji wa TikTok alisema: "Tunatekeleza kwa umakini matumizi yanayolingana na umri wa mtumiaji kupitia kanuni za jukwaa zilizoandaliwa kwa ushauri wa wataalamu na teknolojia za hali ya juu za kukadiria umri, sambamba na kampuni nyingine kubwa katika sekta hio."
Kate Davies, mkurugenzi wa mkakati na utafiti katika Ofcom, aliiambia BBC Radio kuwa mdhibiti huyo ana mashaka kuhusu mfumo wa utambuzi wa umri, ambao mitandao ya kijamii hutumia kukadiria umri wa mtumiaji kulingana na mwenendo wake wa matumizi mtandaoni.
"Njia hiyo haijajumuishwa katika mwongozo wetu kama mbinu madhubuti ya kuthibitisha umri wa mtumiaji," alisema.
Sheria ya Usalama Mtandanoni inalenga kuwalinda watoto dhidi ya kukutana na maudhui hatarishi yanayohusu kujiua, kujidhuru, matatizo ya ulaji wa chakula na picha za ngono.
Pia, kampuni za teknolojia zinatakiwa kuwalinda watoto dhidi ya maudhui yenye chuki dhidi ya wanawake, vurugu, chuki, lugha za matusi au unyanyasaji, pamoja na uonevu wa mtandaoni na changamoto hatari zinazoweza kuhatarisha maisha au afya.
Makampuni yatakayokiuka sheria yanaweza kutozwa faini ya hadi pauni milioni 18 (takriban Dola milioni 24 za Marekani) au asilimia 10 ya mapato yao.
Pamoja na kutangaza uchunguzi wake, Ofcom ilionya katika ripoti kwamba watoto bado wanaweza kutumia mitambo ya mitandaoni kupata "kwa urahisi" tovuti za ngono ambazo hazitumii mfumo wa kuthibitisha umri wa watumiaji.
















