Mpango wa Marekani kuvuna madini kutoka DRC wapingwa
Rais Felix Tshisekedi alitoa ofa kwa makampuni ya Marekani kuchimba na kuvuna madini yenye thamani ya Dola Trilioni 24, kama sehemu ya mpango wa Marekani kuisaidia DRC kupambana na waasi.
Mpango wa Marekani kuvuna madini adimu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), umeendelea kupingwa, siku chache baada ya Rais Felix Tshisekedi kurejea kutoka Marekani.
Tshisekedi alitoa ofa kwa makampuni ya Marekani kuchimba na kuvuna madini yenye thamani ya Dola Trilioni 24, kama sehemu ya mpango wa Marekani kuisaidia DRC kupambana na waasi.
Februari 4 mwaka huu, Rais Tshisekedi aliongoza ujumbe wa watu kadhaa nchini Marekani, kwa ajili ya mfululizo wa vikao na maafisa waandamizi kwenye serikali ya Donald Trump, kwa ajili ya kupanga mikakati ya ushirikiano kuhusu mikataba iliyosainiwa mwezi Desemba mwaka jana.
“Tuko tayari kufanya biashara,” alisema Tshisekedi wakati akiwaambia wajumbe kutoka baraza la biashara la Marekani wiki iliyopita.
Majadiliano hayo, yaliangazia mapitio ya mali za DRC ambazo zitatoa fursa kwa wawekezaji wa Marekani.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo nchini DRC, wanaamini kuwa mkakati huo hautosaidia katika kumaliza mapigano katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.