Kupitia taarifa aliyochapisha kwenye akaunti yake rasmi ya X, Rais wa Kenya William Ruto alisema makubaliano hayo yanaweka msingi wa ushirikiano wa kimkakati na wa vitendo kati ya mataifa hayo mawili, yakilenga kuhakikisha kuwa ahadi za kisiasa zinatafsiriwa katika miradi halisi ya maendeleo. Alisema mpango huo wa miaka mitatu umekubaliwa rasmi kama mfumo wa utekelezaji utakaongoza uhusiano wa Kenya na Italia katika kipindi hicho.
Mazungumzo hayo yalimhusisha pia Rais wa Italia Sergio Mattarella na Waziri Mkuu Giorgia Meloni, ambapo viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika sekta za maendeleo, uchumi na diplomasia.
Katika mazungumzo hayo, Kenya na Italia pia zimeafikiana kuanzisha mfumo rasmi wa mazungumzo ya kisiasa ya mara kwa mara, utakaohusisha mashauriano ya ngazi ya juu kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa, pamoja na uratibu wa sera za amani, usalama na ushirikiano wa kiuchumi duniani.
Ushirikiano huo mpya umejengwa chini ya Mpango wa Mattei kwa Afrika, ambao sasa umewekwa kama msingi mkuu wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Kupitia mfumo huo, Kenya na Italia zitashirikiana katika sekta za nishati, kilimo, miundombinu, viwanda, ajira na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, zikiwa na lengo la kukuza maendeleo endelevu.
Ruto alithibitisha kuwa katika ziara hiyo, mikataba minane imesainiwa, ikihusu sekta ya mazingira, ulinzi na usalama, elimu, utafiti na ubunifu pamoja na mafunzo ya ujuzi. Alisema mikataba hiyo inalenga kuimarisha taasisi na kuongeza uwezo wa kiufundi kati ya mataifa hayo mawili.
Viongozi hao pia walijadili kuimarisha biashara na uwekezaji, huku Kenya ikisisitiza dhamira yake ya kuwa kitovu cha uwekezaji katika Afrika Mashariki kupitia sekta za viwanda, nishati na kilimo. Aidha, ushirikiano umepanuliwa katika teknolojia za kisasa, ikiwemo akili mnemba na utafiti wa anga kupitia Kituo cha Anga cha Luigi Broglio kilichopo katika mji wa Malindi nchini Kenya.
Rais Ruto amesema makubaliano hayo yanaweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu, wenye mwelekeo wa kimkakati na unaolenga matokeo, akieleza kuwa Mpango wa Utekelezaji wa 2026–2029 ni hatua muhimu ya kuhakikisha diplomasia ya Kenya inazalisha matokeo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wake.


















