Afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Iran na Marekani zinapaswa kuruhusu "mara moja" usafirishaji wa mbolea kupitia Mlango-bahari wa Hormuz, ili kupunguza mzozo katika baadhi ya nchi zilizo katika hali tete zaidi.
Jorge Moreira da Silva, mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNOPS), aliambia mkutano wa hali ya hewa wa COP31 nchini Uturuki siku ya Jumamosi kwamba ukosefu wa mbolea unaweza kusababisha mamilioni ya watu kutumbukia katika umaskini.
Kuzuiwa kwa njia hiyo muhimu ya maji na Iran—hatua iliyoanza baada ya shambulio la pamoja la Marekani na Israel dhidi ya Iran mwishoni mwa mwezi Februari—kumeathiri sana usafirishaji wa meli katika eneo hilo na kwingineko.
Vilevile, hatua ya Marekani ya kuzuia bandari za Iran imezidisha utata wa hali hiyo.
Wakati Iran na Marekani zikiendelea kujaribu kufikia makubaliano ya kumaliza mzozo huo, Moreira da Silva alisema ana ujumbe mmoja kwa nchi zote mbili.
"Zinapaswa kuendelea na mazungumzo kuhusu makubaliano ya kina, lakini makubaliano hayo hayapaswi kupuuza utafutaji wa suluhisho la haraka, la kipekee, lenye mipaka, na la muda maalum kwa ajili ya mbolea," alisema.
"Kimsingi, tunachohitaji ni meli tano zenye mbolea kwa siku," aliongeza.
Mamilioni wako hatarini
Moreira da Silva anaongoza kikosi kazi cha Umoja wa Mataifa kilichoundwa ili kuwezesha usafirishaji salama wa mbolea wakati wa mzozo huu.
Alisema kuwa kabla ya mzozo huo, theluthi moja ya mbolea duniani ilipitia katika Mlango-bahari wa Hormuz, na tangu kuanza kwa vizuizi hivyo, bei ya mbolea imepanda kwa asilimia 30.
"Lakini nadhani jambo ambalo halijatiliwa maanani ipasavyo ni athari kubwa isiyo na uwiano kwa nchi zilizo katika hali tete zaidi," aliongeza.
Alieleza kuwa Waziri wa Fedha wa Sudan hivi karibuni alimwambia kuwa bei ya chakula nchini humo imeongezeka maradufu katika kipindi cha miezi sita.
Nchini Nepal, alielezwa kuwa wakulima hawana tena uwezo wa kununua mbolea.
"Hivyo, ni muhimu sana kufahamu kuwa nchi kama Msumbiji, Kenya, Sudan, Somalia, Nepal, Bangladesh, na Sri Lanka zinakabiliwa na athari kubwa sana."
Alionya kuwa madhara ya uhaba huu yanaweza kuwa mabaya mno.
"Ikiwa tutaendelea kukosa misimu ya upandaji katika sehemu mbalimbali duniani, huenda tukawa na watu milioni 45 wanaokabiliwa na uhaba mkubwa na wa dharura wa chakula," alisema.
"Huenda tukawa na watu milioni 30 wanaolazimishwa kuingia katika umaskini."
Alisema Umoja wa Mataifa una mfumo tayari wa kuwezesha usafirishaji wa mbolea kuanza ndani ya siku saba hadi kumi.






















