Moto katika uwanja wa ndege wa Cape Town nchini Afrika Kusini wasitisha safari kadhaa

Moto ulizuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cape Town siku ya Jumanne, na kusababisha abiria kuhamishwa pamoja na kuvuruga safari za kimataifa za kwenda na kutoka katika mji maarufu wa kitalii wa Cape Town.

By
Moto ulozuka katika uwanja wa ndege wa Cape Town, Afrika Kusini mnamo Februari 24, 2026. / / TRT Afrika Swahili

Picha zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha wasafiri wakiondoka haraka katika uwanja huo wa ndege, wakiwa na masanduku yao, huku moshi ukijaa ndani ya jengo la abiria na ving’ora vikilia kutoa tahadhari ya uhamishaji wa dharura.

“Kampuni ya Viwanja vya Ndege Afrika Kusini (ACSA) inathibitisha kuwa kulitokea moto,” ilisema katika taarifa, ikiongeza kuwa moto huo “umezimwa” na hakuna mtu aliyejeruhiwa.

“Kama hatua ya tahadhari, safari za kimataifa za kuondoka zimesitishwa kwa muda, na ndege za kimataifa zinazoingia zinaelekezwa katika viwanja vingine,” ilisema taarifa hiyo, ikibainisha kuwa moto huo uliathiri “huduma za mtandao.”

Maboresho ya uwanja wa ndege

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, safari za ndege za kimataifa ambazo tayari zilikuwa zimetua ziliendelea kushughulikiwa kama kawaida.

Moto huo umetokea siku chache tu baada ya kutangazwa kwa mradi mkubwa wa maboresho ya miundombinu ya uwanja huo wa ndege, utakaotekelezwa kwa awamu.

Kulingana na takwimu za ACSA, Uwanja wa Ndege wa Cape Town ulihudumia abiria milioni 11.1 mwaka 2025, wakiwemo wasafiri wa kimataifa milioni 3.33.