Erdogan aonya kuhusu migogoro ya dunia, ataka diplomasia, utulivu wa kikanda
Rais Erdogan amesema dunia inakabiliwa na "hatari," ametaka diplomasia kutumika katika migogoro, na amejitolea Uturuki kuwa kitovu cha mazungumzo ya amani wakati wa migogoro ya kikanda na kimataifa.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametahadharisha kwamba ulimwengu unakabiliwa na mgogoro mkubwa wa utawala na muongozo, na kutaka kuwepo kwa dhamira mpya ya diplomasia, mazungumzo na ushirikiano kwa misingi ya sheria wakati ambapo wasiwasi duniani unaongezeka.
Akizungumza katika ufunguzi wa Jukwaa la Diplomasia la Antalya Ijumaa, Erdogan amesisitiza kwamba migogoro ya katika kanda, kuanzia Gaza hadi Ukraine, inaonesha kufeli kwa mifumo iliyopo duniani na umuhimu wa kuwepo kwa mabadiliko na hatua jumuishi.
Mkutano huo wa siku tatu, unaofanyika chini ya kauli mbiu, “Kutathmini Yajayo, Kukabiliana na Yasiyo na Uhakika,” umeleta pamoja viongozi wa dunia na maafisa waandamizi kusini mwa Uturuki kujadili kukosekana kwa hali ya utulivu katika mazingira yanayobadilika.
Tahadhari ya mgogoro wa dunia
Erdogan amesema mfumo wa kimataifa sio tu unabadilika lakini pia unakabiliwa na "mgogoro wa muelekeo" na kuonya kwamba dunia imefikia "kiwango kibaya zaidi."
Amekosoa taasisi ya ulimwengu kwa kushindwa kutenda haki na kulinda raia, na kusema mifumo iliyopewa jukumu la kulinda haki za binadamu imeshindwa kuchukua hatua na wakati mwengine kutofautiana panapotokea ukiukwaji mkubwa.
Ameelezea mgogoro wa sasa, akigusia Syria, Gaza, na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Lebanon kama mifano ya kufeli kwa mfumo.
Gaza na mfumo wa dunia
Rais wa Uturuki amesema hali ya Gaza inawakilisha zaidi janga kwa watu, akiielezea kama mauaji ya halaiki ambayo yamedhihirisha mipaka na ubaguzi wa mfumo wa sasa wa ulimwengu.
Amehoji ni jinsi gani uaminifu utapatikana katika mfumo ambao umeshindwa kuzuia mateso ya raia na ukiukaji wa halaiki, na kuitaka jumuia ya kimataifa kukabiliana na kile alichokiita kuporomoka kwa uwajibikaji wa maadili.
Erdogan aliongeza kuwa mifumo ya dunia ya utawala bora lazima ifanyiwe marekebisho kuhakikisha uwajibikaji na usawa.
Diplomasia katika mgogoro
“Haijalishi mgogoro ni mkubwa kiasi gani, katu tusiruhusu matumizi ya silaha kuchukua nafasi ya mazungumzo," amesema Erdogan, akitilia mkazo dhamira ya Uturuki kwa sera ya mambo ya nje ya amani.
Amesisitiza utayari wa Uturuki kuratibu mazungumzo katika migogoro inayoendelea, ikiwemo uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine, na hata mkutano wa viongozi, iwapo mazingira yataruhusu.
Uturuki, amesema, inaendelea kujiweka katika nafasi ya upatanishi kwa kuweza kuunganisha pande zilizogawanyika na kutafuta suluhu ya kidiplomasia.
Shinikizo la utulivu wa kikanda
Erdogan amesisitiza kwamba utulivu katika nchi jirani ya Syria unabaki kuwa muhimu kwa mustakabali wa kikanda, na kutaka kuwepo kwa jitihada endelevu za amani, kurudisha hali ya utulivu na ujenzi mpya.
Ameelezea lengo la Uturuki la kuirudisha Mashariki ya Mediterania na Aegean kuwa eneo lenye utulivu, na kukataa hatua za pamoja ambazo zitaitenga Uturuki na Jamhuri ya Kituruki ya Kupro Kaskazini.
Ameongeza kusema kuwa, Uturuki iko wazi kwa ushirikiano na nchi majirani katika sekta ya nishati na miradi ya mawasiliano.
Kujitika katika ulinzi wa majini
Akizugumzia kuhusu kuongezeka kwa hali ya wasiwasi inayohusiana na Iran, Erdogan amesisitiza kwamba uhuru wa kusafiri lazima uwepo, huku akitaka Mlango Bahari wa Hormuz ubaki wazi kwa meli za kibiashara.
Amesisitiza kwamba nchi za Ghuba lazima ziruhusiwe kufikia bahari, na kuonya kwamba kutatizika kwa aina yoyote katika njia ya bahari kutakuwa na athari kubwa ya uchumi wa dunia.
Umoja wa Ulaya na muungano
Erdogan amethibitisha tena lengo la muda mrefu la Uturuki kutaka kuwa mjumbe wa Umoja wa Ulaya, akionesha matumaini kwamba jumuia hiyo itakabiliana na kile alichokiita “mgogoro wa muelekeo” na kurudi katika misingi yake ya uanzilishi.
Pia amegusia umuhimu wa kuimarisha miungano huko kukiwa na mizania huru katika sera za kigeni.
Jukwaa la Diplomasia la Antalya, huu ni mwaka wake wa tano, na limekuwa Jukwaa muhimu katika mazungumzo ya kimataifa, likileta pamoja watunga sera, wanadiplomasia, na wabobezi kujadili changamoto za dunia.
Erdogan ameuelezea mkutano huo kama fursa sio tu ya kutatua migogoro lakini pia kuweka misingi ambayo itaongoza maisha ya baadae katika uhusiano wa kimataifa.
Ameonesha matumaini yake kwamba majadiliano katika Jukwaa hilo yatachangia katika safari pana ya Uturuki ya kuleta amani, utulivu na ushirikiano duniani.